Jumatano, 23 Machi 2022

PAC YARIDHISHWA NA UJENZI WA IJC ZA TEMEKE NA KINONDONI

Na Tiganya Vincent, Mahakama

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imeridhishwa na jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyotumia fedha katika utekelezaji wa miradi miwili ya Ujenzi wa Vituo Jumuishi wa Utoaji Haki (Integrated Justice Centres-IJCs) za Temeke na Kinondoni.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 23 Machi, 2022 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japhet Hasunga wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea Mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Temeke na Kinondoni.

‘Baada ya mahojiano na ukaguzi wa miradi yote miwili, Kamati imeridhika kuwa thamani ya fedha iliyotumika inalingana na miradi iliyotekelezwa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo hayo,” amesema Mhe. Hasunga.

Mhe. Hasunga ameongeza kuwa fedha hizo zimetumika kujenga majengo na kuimarisha mifumo ambayo inasaidia katika kuharakisha utoaji haki kwa wananchi katika mazingira rahisi.

Aidha; Kamati imepongeza pia Mahakama kwa kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) katika utoaji haki na uhifadhi wa nyaraka mbalimbali ambapo wananchi wamesogezewa huduma.

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Geophrey Pinda amesema ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJC) umesaidia kusogeza huduma na kuwafikia wananchi wengi kwa urahisi.

Amesema Serikali iko katika mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuiwezesha Mahakama kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika Kanda 12 zilizobaki ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa karibu.

“Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vimekuwa kimbilio kubwa kwa wananchi ambapo kwa Temeke pekee kwa siku wanapokea wananchi Zaidi ya 400 ambao wanakwenda kupeleka mashauri mbalimbali,” amesema Mhe. Pinda.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wamefanikiwa kujenga Vituo Jumuishi 6 katika Mikoa mitano kwa gharama ya shilingi bilioni 51.5.

Amesema Vituo hivyo viko katika Mkoa wa Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Arusha, Morogoro, Mwanza na Dodoma.

Prof. Ole Gabriel amesema katika IJC kuna Mahakama ya Mwanzo hadi ya Rufaa na pia zipo Ofisi za wadau mbalimbali kama vile Maafisa wa Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Ofisi za Mawakili wa Kujitegemea na wengine ambao wakatika mnyoro wa utoaji haki.

Kamati inatarajia kuendelea na ziara yake ya ukaguzi wa Mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Morogoro mwishoni mwa Mwezi huu.

Mwenyekiti wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Japhet Hasunga (katikati) akizungumza katika kikao kati ya Mahakama na Kamati hiyo. Kamati hiyo imeonyesha kuridhishwa na matumizi sahihi ya fedha katika Miradi ya Ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vya Temeke na Kinondoni mara baada ya kuvikagua leo tarehe 23 Machi, 2022. Kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakiwa katika kikao mara baada ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Temeke. Wajumbe hao wameonyesha kuridhishwa na ubora wa Vituo Jumuishi vya Temeke na Kinondoni na kusema kuwa gharama iliyotumika inaendana na ubora wa majengo hayo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo wakati wa kikao hicho, kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda, wa pili kulia ni  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Mary Makondo na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Japhet Hasunga.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda akichangia jambo katika kikao hicho.
Picha mbalimbali za ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ilipofanya ukaguzi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke leo tarehe 23 Machi, 2022.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Katiba na Sheria, Mhe. Isack Kamwelwe (aliyesimama mbele) akiwa na wajumbw wenzake katika moja ya kumbi za Mahakama zilizomo katika jengo la IJC Temeke.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (aliyenyoosha mikono) akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali walipokuwa wakikagua Mradi wa Ujenzi wa IJC Temeke.
Sehemu ya Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo vya Mahakama walioshiriki katika kikao pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni