Jumatano, 30 Machi 2022

UKATILI DHIDI YA WATOTO HAUVUMULIKI: JAJI NGWEMBE

 Na Evelina Odemba - Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amelaani vikali ubakaji na ulawiti kwa watoto ambao umekithiri katika jamii ambapo ameonya vitendo hivyo havitavumiliwa.

Mhe. Ngwembe ametoa msimamo huo jana tarehe 29 Machi, 2022 alipokuwa akitoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi ambao walifika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani hapa kupata huduma za  Mahakama.

Mahakama Morogoro imeanzisha utaratibu wa kutoa elimu kwenye masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi siku za Jumanne, Jumatano na Alhamisi kuanzia saa 2.00 mpaka saa 3.00 asubuhi kabla ya kuanza shughuli za kimahakama ambapo siku ya jana mada ilihusu ulinzi kwa mtoto.

Akizungumza na wananchi waliofurika kwenye Kituo hicho kwenye kipindi cha utoaji wa elimu, Mhe. Ngwembe alisema kuwa amefanya utafiti mkoani Morogoro na kugundua uwepo wa wimbi kubwa la matukio ya ubakaji kwa watoto chini ya umri wa miaka 18.

Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi huyo, takwimu zinaonesha kwa mwaka 2021 mashauri yaliyofikishwa mahakamani yanayohusu ubakaji wa watoto chini ya miaka 18 yanafika 200 na kati ya hayo mashauri 35 yanahusisha ulawiti kwa watoto na hayo ni kwa Mkoa wa Morogoro peke yake.

“Matukio haya ni ya kikatili na aibu kubwa, hayavumiliki katika jamii na jambo hili linakemewa vikali hata katika Mihimili ya Dora nchini ikiwemo Bunge, Serikali na Mahakama, hivyo kila mmoja katika jamii anawajibika kumlinda mtoto mahali kokote anapokuwa,” alisema.

Mhe. Ngwembe alikumbushia kuwa ikibainika mtu yeyote ametenda kosa la namna hiyo hupata adhabu kubwa inayoanzia kifungo cha miaka 30 au kifungo cha maisha jela bila kusahau adhabu zingine ikiwemo kuchapwa viboko.

Hivyo, Jaji Mfawidhi huyo amewaasa wananchi wote kujiepusha na vitendo hivyo ili kuwalinda watotot na kutotumbukia kwenye madhira ya kukumbana na adhabu kali zinazotolewa na Mahakama kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Akimjibu mwananchi mmoja baada ya kutoa nafasi ya kuuliza maswali, Mhe. Ngwembe aliionya jamii kutowatumia watoto kutoa ushahidi wa uongo mahakamani kwa lengo la kulipiza kisasi au chuki kwa watuhumiwa kwani ikigundulika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya walalamikaji.

Mwananchi huyo alieleza changamoto ambayo hujitokeza kwa baadhi ya watu kutunga ushahidi kwa lengo la kukomoa au kulipiza kisasi, hivyo alitaka kujua hatua zinaweza kuchukuliwa kwa kubambikiwa kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (picha ya juu na chini) akizungumza na wananchi walifurika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki wakati akitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria kabla ya kuanza shughuli za kimahakama jana tarehe 29 Machi, 2022.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni