Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Mahakama ya Tanzania
imeandaa mpango mahsusi wa kushindanisha viwango vya utoaji huduma kwa wananchi
ili kupata Mahakama ambayo ni bora katika utendaji kazi (Court of Excellence
Performance).
Hayo yamebainishwa na
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athumani
Matuma wakati akiongea na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kahama jana tarehe 29
Machi, 2022 katika siku ya pili ya ziara yake kukagua shughuli mbalimbali za
kimahakama.
Mhe. Matuma
amewafahamisha watumishi wa Mahakama hiyo kuwa kuna vigezo ambavyo vimeandaliwa
vitakavyotumika kushindanisha ubora wa huduma zotolewazo kati ya Mahakama moja
na nyingine ambapo mshindi atatambuliwa na kutangazwa.
Amewataka watumishi kutambua
kuanzia sasa huduma wanazotoa katika maeneo yao ya kazi zitapimwa kwa vigezo
maalum vilivyoainishwa katika muongozo kupima utendaji kazi bora wa kila Mahakama
ambapo ile itakayofanya vizuri itatambuliwa na kupewa cheti maalum katika ngazi
ya Kitaifa.
Kadhalika, Mhe. Matuma
amewafahamisha watumishi kuwa, pamoja na kushindanishwa kitaifa, kutakuwa na
ushindani ndani ya Kanda ambapo mshindi anayefanya vizuri katika kutoa huduma
bora atatambuliwa na kupewa tuzo maalum.
“Kila mmoja wenu afahamu
sasa anayo kazi ya kuhakikisha Mahakama anayofanyia kazi inakuwa ya kwanza
katika utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” alisema Jaji
Mfawidhi huyo.
Jaji Matuma amebainisha
baadhi ya vigezo vitakavyotumika kupima utendaji bora ni kiwango cha kusikiliza
na kumaliza mashauri kwa wakati, kumaliza mlundikano wa mashauri mahakamani,
kusikiliza na kutatua malalamiko ya wananchi kwa haraka na kuhuisha takwimu za mashauri katika mfumo wa
JSDS II.
“Hivyo ni fursa kwa
kila Mtumishi kujipima na kujitathmini na kuona kuwa kila mmoja ana mchango
mkubwa katika kufikia utendaji kazi bora katika eneo lake,” amesema.
Kwa upande wao, watumishi
wa Mahakama hiyo wamemuahidi Mhe. Matuma kuwa watafanya kazi kwa nguvu zao zote
na kwa ubora unaohitajika ili kuifanya Mahakama ya Wilaya ya Kahama kuwa mfano kwa
Mahakama zilizopo Kanda ya Shinyanga na nyinginezo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga, Mhe Athuman Matuma (katikati) akifafanua jambo wakati wa kikao na
watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kahama. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama
Kanda ya Shinyanga, Mhe. Hussein Mushi na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama katika
Kanda hiyo, Bi Mavis Miti.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama ambao wameahidi
kufanya vizuri kuboresha huduma za Mahakama katika Wilaya ya Kahama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga,
Mhe. Athuman Matuma akikagua uchapaji wa mienendo ya mashauri katika Mahakama
ya Wilaya ya Kahama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni