Alhamisi, 24 Machi 2022

USIKILIZAJI MASHAURI KWA NJIA YA MTANDAO WASHIKA KASI KASULU

 Na Festo Sanga-Mahakama, Kigoma

Usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao umeshika kasi mahakamani kufuatia hatua aliyoifanya jana tarehe 23 Machi, 2022 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha kuzindua huduma hiyo katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu.

Usikizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao una manufaa lukuki, ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji zinazohusisha usafirishaji wa mashahidi na washtakiwa kutoka Kambi ya Nyarugusu kwenda Kasulu na Kigoma kufuata huduma za Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu.

Akifungungua huduma hizo, Jaji Mlacha aliwataka Mahakimu kusikiliza mashauri ya maombi na rufaa kwa njia ya mtandao pamoja na yale yanayoanza (Original jurisdiction) isipokuwa katika mazingira ambayo shahidi anapaswa kutoa kielelezo ndipo atakapolazimika kufika Mahakamani.

“Shahidi anayetaka kutoa kielelezo atalazimika kufika mahakamani wakati tunasubili uboreshaji wa kanuni za usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kutegua kitendawili hiki,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.

Amesema ufunguzi wa huduma hizo umefanyika kwa vile Wakimbizi hulazimika kuombe vibali kutoka nje ya kambi na kusafirishwa umbali wa Kilomita 120 kwenda wilayani Kasulu. 

Ili kuondoa kadhia hiyo uongozi wa kambi hiyo kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC) walijenga kituo maalum na kukiwekea huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na pia kufungua mashauri kwa njia hiyo.

Awali akizungumza kabla ya ufunguzi huo, Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu, Bw. Siasa Manjenje alimfahamisha Jaji Mfawidhi kuwa maelekezo aliyoyatoa kuandaa kituo hicho ili kuanzisha huduma za kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao yametekelezwa na kwamba kambi hiyo ipo salama.

 Aidha aliuomba uongozi wa Mahakama kukifanya kituo hicho kuwa Mahakama kutokana na kuwepo kwa miundombinu mizuri  ya TEHAMA. Alieleza kuwa eneo hilo lina wakimbizi 130,134 wakiwemo Wakongo 80,000 Warundi ni 50,000 na mataifa mengine ni 134.

Mkuu wa Kambi hiyo alibainisha pia kuwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo watapata huduma za kimahakama kwa urahisi kwenye kituo hicho ambacho kina miundombinu ya kisasa.

Naye Mkuu wa WLAC Kasulu, Bi Lulu Mshana  ameupongeza uongozi wa Mahakama kwa kuzindua huduma hizo ambazo zitawapunguzia gharama za uendeshaji wa mashauri  na pia mashauri ya ukatili wa kijinsia yatakuwa yakisikilizwa kwa wakati.

Aliongeza kuwa awali watu wengi walikuwa wanakata tamaa kufuatilia mashauri yao kutokana na umbali uliopo wa kufuata huduma za Mahakama katika Mahakama za Kasulu, Kibondo, Kigoma na Mahakama Kuu Kigoma.

“Sisi WLAC kwa niaba ya shirika linalohudumia wakimbizi (UNHCR) tunaupongeza uongozi wa Mahakama kwa kusogeza huduma za utoaji haki karibu na jamii na tutaendelea kutoa ushirikiano katika maeneo mbalimbali na tuko tayari kujifunza,” alisema Bi Mshana.

Katika ziara hiyo ya uzinduzi wilayani Kasulu, Jaji Mfawidhi aliongozana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na Mtendaji wa Mahakama katika Kanda hiyo, Bw. Moses Mashaka.

Ufunguzi wa huduma hizo unatokana na uwepo wa kanuni za usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ‘The Judicature and Application of Laws (Remote Proceedings and Electronic Recording Rules)’ ili kutekeleza dira ya Mahakama ya utoaji wa haki kwa wakati.  
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (katikati) akifanya  majaribio ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kati ya mtandao wa Mahakama ya Wilaya Kasulu na uliopo Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu- Kasulu. Wanaoshuhudia tukio hilo lililofanyika tarehe 23 Machi, 2022 ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki (kushoto) na kulia ni Mtendaji wa Mahakama wa Kanda hiyo, Bw. Moses Mashaka.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (kushoto) na Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu, Bw. Siasa Manjenje (kulia) wakifuatilia tukio hilo la majaribio ambapo walijiridhisha kuwa mashauri yanaweza kuendelea kusikilizwa kwa njia ya mtandao.


Majaribio ya mtandao yakifanyika kati ya Kambi ya Nyarugusu Kasulu na Mahakama ya Wilaya Kibondo na Kasulu. Viongozi wa Mahakama na Uongozi wa shirika la WLAC wakishuhudia tukio hilo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu- Kasulu na viongozi wa Mahakama mara alipotembelea kituo hicho na kukizindua tarehe 23 Machi 2022.


Jengo lililojengwa katika Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu- Kasulu kama kituo maalumu kwa ajili ya kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao ambalo uongozi wa Kambi hiyo wameomba liwe Mahakama ya Mwanzo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni