Alhamisi, 24 Machi 2022

JAJI MFAWIDHI MUSOMA AWAPONGEZA MAHAKIMU KWA USHIRIKIANO NA VIONGOZI SERIKALINI

 Na. Francisca Swai – Mahakama, Musoma

Ziara ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama imeingia siku ya sita leo tarehe 24 Machi, 2022 ambapo amewashukuru Mahakimu kwa ushirikiano wanaotoa kwa viongozi wa Kata, Vijiji au hata Wilaya kwani kwa kufanya hivyo hudumisha amani, umoja na kujenga mazingira rafiki ya utendaji kazi.

Katika ziara yake, Jaji Mtulya amekutana na viongozi mbalimbali wa Kata ya Bugoji na Nyambono alipotembelea na kukagua Mahakama ya Mwanzo Nyambono iliyojengwa mwaka 1954, umbali wa Kilomita 60 kutoka Musoma Mjini inayohudumua jumla ya Kata saba za Nyambono, Bugoji, Msanja, Bugwema, Nyamrandirira na Suguti.

Jaji Mfawidhi huyto alifanya mazungumzo na Waheshimiwa Madiwani wa Kata hizo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambono, Mtendaji wa Kata ya Nyambono pamoja na viongozi wa chama na serikali waliofika kumsalimia alipokuwa katika ziara hiyo.

Mhe. Mtulya aliwaasa viongozi hao kuendeleza ushirikiano uliopo na Mahakama katika mambo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo mpango wa kuweka umeme, maji, upimaji wa viwanja pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za kimahakama kwani Mahakama kama zilivyo shule na zahanati nayo inatoa huduma kwa watanzania wote.

Katika ukaguzi wa Mahakama hiyo, Jaji Mfawidhi huyo aliridhishwa na utendaji kazi wa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Baraka Kajiru ambaye viongozi hao walimwelezea kuwa mtumishi mwenye nidhamu, msikivu na hutoa ushirikiano mkubwa pale anapohitajika katika shughuli mbalimbali za Kijiji.

Aidha katika ziara yake, Mhe. Mtulya pia alikagua Mahakama za Mwanzo Bukwaya, Mugango, Nyambono na Musoma Mjini ambapo aliwapongeza watumishi kwa utendaji kazi mzuri wa kuridhisha licha ya changamoto zilizopo kama vile uchakavu wa majengo, uhaba wa watumishi na vitendea kazi pamoja na uvamizi wa baadhi ya maeneo ya Mahakama.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Bw. Chonya alimhakikishia Jaji Mtulya pamoja na watumishi kuwa kwa kushirikiana na Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) zilizoko Musoma Mjini watapata miti ya kutosha kupanda kuzunguka maeneo yote ya Mahakama, Kanda ya Musoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Bukwaya, Mhe. Pendo Bissaya (kushoto) pamoja na watumishi wengine wa Mahakama hiyo.

Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Mugango, akiwemo Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Gibson Ngojo (wa pili kulia) wakipokea vitendea kazi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto) alipotembelea na kukagua Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akitoa vitendea kazi kwa watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Bwasi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja ya viongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma, viongozi wa Mahakama ya Wilya Musoma, watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Nyambono pamoja na viongozi mbalimbali wa eneo la Nyambono na Bugoji.

Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa tano kulia).

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mhe. Prisca Mkeha akisoma taarifa ya utendaji kazi mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.

Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni