Na Charles Philipo Ngusa- Mahakama Geita.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Jaji
John Kahyoza amepongeza
juhudi zinazoendelea kufanywa na Mahakimu katika Mkoa wa Geita, hususani katika
kusikiliza mashauri kwa haraka, hivyo kutekeleza kwa vitendo azima ya Mahakama
katika kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.
Akizungumza na watumishi
mkoani humo Mhe. Kahyoza amesema kuwa pamoja na mkakati uliowekwa na Kanda wa kumaliza
mashauri katika Mahakama za Mwanzo ndani ya miezi mitatu, wao wameenda mbali zaidi
kwa kujiwekea malengo kumaliza mashauri katika Mahakama hizo ndani ya mwezi
mmoja, jambo ambalo wameliweza, hivyo kuwa mfano ndani ya Kanda hiyo.
“Mashauri mengi ndani
ya Mkoa huu yamekuwa yakimalizika ndani ya wiki moja, jambo ambalo limewafanya
wananchi kuona kuwa Mahakama imekuwa kimbilio la watu kwani mashauri yao
yanamalizika haraka na kuruhusu waendelee na majukumu yao mengine,” alisema
wakati alipokuwa kwenye ziara ya siku nne iliyoanza tarehe 28 Machi, 2022.
Alibainisha kuwa
Mahakimu hao wamekubaliana shauri linapowasilishwa mahakamani kabla halijakubaliwa lazima mashahidi na
wahusika wawepo na mara baada ya kufunguliwa huanza kusikilizwa siku hiyo na
kutolewa hukumu au uamuzi kwa haraka ili kila mmoja apate haki yake, hivyo
kutoa fursa kwa wahusika kwenda kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.
“Kwa kufanya hivyo
wameifanya Mahakama kuwa kimbilio la watu kwani wanaamini wakifika mahakamani
mashauri yao yanamalizika ndani ya muda mfupi bila kupoteza muda wao,” Mhe.
Kahyoza alisema.
Akiwa katika ziara
yake, Jaji Mfawidhi huyo alipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa Wilaya ya Geita,
Mhe. Wilson Shimo, ambaye alimpongeza Mhe. Kahyoza kwa kusimamia maadili na uchapaji
kazi ulio bora kwani kwa sasa Mahakimu wamekuwa wakitekeleza majukumu yao
kikamilifu.
“Hatua hii imepunguza
malalamiko katika ofisi yangu ikilinganishwa na siku za mwanzo ambapo tulikuwa
tukipokea malalamiko mengi sana ndani ya wiki moja lakini kwa sasa tunaweza
kupokea lalamiko moja au hamna kabisa,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kadhalika, Mhe. Shimo
alisema kuwa kutokana na wananchi kuridhishwa na huduma za kimahakama, wamekuwa
na mwamko mkubwa katika ushiriki wa shughuli mbalimbali za Mahakama kama vile
ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Jaji John Kahyoza (aliyesimama) akielezea
jambo kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya Chato(hawapo pichani),akiwemo Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mhe. Amalia Mushi (kushoto) na Naibu Msajili Mfawidhi, Kanda ya
Mwanza, Mhe. Chiganga Tengwa(wa pili kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa
Geita, Bw. Nestory Mujunangoma(kulia).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza,
Mhe. Jaji John Kahyoza (kulia) akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita,
Mhe. Wilson Shimo (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake wakati alipokuwa
kwenye ziara yake ya Mahakama kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Mwanza, Mhe. Jaji John Kahyoza (katikati) akiwa na baadhi ya watumishi wa
Mahakama ya Mwanzo Katoro wakati wa ziara yake.
Watumishi katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Geita wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Mwanza, Mhe. Jaji John Kahyoza katika
kikao cha majumuisho cha ziara yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni