Na Angel Meela-Mahakama, Arusha
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu amewahimiza Mahakimu
Wakazi Wafawidhi kuendelea kuzingatia maadili na Nnidhamu ya hali ya juu
wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe.
Mdemu alitoa wito huo jana tarehe 1 Aprili, 2022 alipokuwa akifungua mafunzo ya
siku mbili kwa viongozi hao wa Mahakama yanayofanyika katika ukumbi wa Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha. Jaji Mdemu alimwakilisha Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani katika ufunguzi huo.
Alisema
ni ukweli usiopingika kwamba uadilifu ndio chachu ya mafanikio na utendaji bora
katika sehemu yeyote ya kazi, hivyo maadili na nidhamu kwa mtumishi ni muhimu
kwa mustakabali wa taasisi inayotarajia mafanikio, kwani mambo hayo hujenga
imani kwa wadau wake.
“Kwa
vyombo vya utoaji haki kama Mahakama kukosa uadilifu hupelekea kuvunjika kwa
imani ya wananchi na hivyo kuathiri dhana nzima
ya utawala na sheria. Hivyo basi kujenga
na kuimarisha maadili ya maafisa wa mahakama ni jukumu la msingi la taasisi
ya Mahakama kama ilivyo kwa taasisi nyingine yeyote duniani,” Jaji Mfawidhi huyo
alisema.
Akinukuu
maneno ya mwanazuoni mmoja na Rais wa
Mahakama ya Katiba ya Poland kuhusu maadili Mhe. Mdemu alisema, "kuwa
Hakimu au Jaji ni nafasi nzuri na inayopendwa kama ilivyo kuwa daktari au
mwanazuoni.
“Lakini
Ujaji au Uhakimu sio kazi nzuri kwa watu wasio na maadili ya kitaaluma au
binafsi, uaminifu, historia safi ya maisha yao ya nyuma, ujuzi wa taaluma na
utendaji bora, ukomavu binafsi, kifamilia na jamii kwa ujumla, ili kuweza
kuwajibika kwa kila maamuzi wanayotoa kulingana na sheria na dhamira zao binafsi."
Jaji Mfawidhi
huyo aliendelea kwa kusema kuwa ni dhahiri mtu anaefanya kazi ya Uhakimu hana
budi kuishi maisha ya kujizuia, kinyume na mtu mwingine wa kawaida kwa vile jamii
inatarajia Jaji au Hakimu kuwa mtu mwenye kiwango cha juu kabisa cha uadilifu
ili aweze kuaminika katika kazi yake ya kutoa haki.
“Hivyo ninyi
kuchagua kuwa Mahakimu, mmekubali pia kuwa maisha yenu hatatakua binafsi.
Wananchi wana haki ya kufuatilia mienendo yenu na kutoa maoni iwapo
hawajaridhika na mienendo yenu,” alisema.
Mhe. Mdemu alieleza kuwa maadili ya Mahakimu ni eneo pana ambalo linahusu maisha ya kila
siku wakati wa kazi. Mhe Jaji aliwakumbusha kwamba suala la maadili ya maafisa
wa Mahakama ni mojawapo ya vipaumbele katika progamu ya uboreshaji wa Mahakama Tanzania
unaolenga kujenga imani ya wananchi na ushiriki wa wadau.
Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni