Na Mayanga Someke – Mahakama, Sumbawanga.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde
ametoa
rai kwa wadau wote wa Haki Jinai Mkoa wa Rukwa kushirikiana ili kumaliza mlundikano
wa mashauri yaliyopo mahakamani.
Akizungumza katika kikao
cha kusukuma mashauri kilichofanyika hivi karibuni kwenye ofisi yake, Mhe.Kasonde aliwaaasa wadau wote kutimiza
wajibu wao ili kutokwamisha mnyororo wa upatikanaji haki pindi mashauri yanapokuwa
yamewasilishwa mahakamani.
“Ninyi
nyote mliopo hapa hakikisheni mnashirikiana ili kuharakisha upatikanaji wa haki
kwa wakati kwa wananchi. Mahakama
peke yake haiwezi
kufanya kazi bila kushirikiana na wadau wengine. Mmoja wenu atasababisha wengine
kukwama kama atashindwa kutimiza wajibu wake,” alisema.
Aliwaambia wadau hao
kuwa ni aibu kuona mashauri yamekwama kusikilizwa kwa sababu mmoja ameshindwa kutimiza
wajibu wake, hivyo ni muhimu kushirikiana kwa pamoja ili mashauri hayo yamalizike
kwa haraka.
“Lazima tufanye kazi kwa
maslahi mapana ya utoaji haki kwa wadau wetu ili kulinda taswira na heshima ya Mahakama,”
alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
Mkoa wa Rukwa,
Bi.
Veronica Myovela aliwaambia
wajumbe wa kikao hicho kuwa wameweka
mikakati yao hadi kufikia tarehe 30 Aprili,2022 upelelezi wa kesi zilizokuwa
zikijadiliwa utakuwa umekamilika.
Naye Kaimu Mkuu wa Waendesha Mashtaka katika Mkoa
huo, Bw, Simon Peres amewahakikishia
wadau wa haki jinai kuwa maazimio yote yaliyofikiwa na Kikao hicho yanayohusu Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka yatatekelezwa kikamilifu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni