Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma amemtaka Mkandarasi
anayejenga Mahakama za Wilaya ya Itilima na Busega Mkoani Simiyu kukamilisha kazi
hizo kwa wakati na kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa Mkataba.
Akiongea na Wasimamizi
wa Mkandarasi huyo, United Builders Limited (UBL), katika ziara ya kukagua miradi
hiyo tarehe 30 Machi, 2022, Mhe. Matuma amehimiza kukamilishwa kwa wakati ujenzi
wa Mahakama hizo ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Amesema hatua hiyo itatoa
fursa kwa wakazi wa Wilaya husika kupata huduma za kimahakama katika maeneo yao
tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wanalazimika kusafiriki umbali mrefu na
kutumia gharama kubwa kutafuta haki katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
‘’Lengo la Jaji Mkuu wa
Tanzania ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kimahakama katika maeneo
wanayoishi pasipo usumbufu na bila gharama yoyote’ alisema Jaji Matuma.
Aliwaeleza Wasimamizi
wa Mkandarasi huyo kwenda na kasi ya Mahakama ya kutoa huduma kwa wananchi kwa
wakati na kwa kiwango kinachoridhisha, hivyo anatakiwa kutumia nguvu zake zote
ili kuikamilisha kazi hiyo kwa haraka.
‘’Mkandarasi aongeze
nguvu kazi kwa kuwa muda wa mkataba uliobaki ni mchache ikilinganishwa na nguvu
kazi iliyopo hivi sasa,’’ aliongeza Jaji Matuma.
Aidha, Jaji Mfawidhi huyo
alimuagiza Hakimu Mkazi Mfawidhi na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu
kusimamia kwa karibu makubaliano ya ujenzi wa Mahakama hizo na kuhakikisha
unakamilika mwezi Aprili, 2022 kulingana na Mkataba ili Mahakama hizo zianze
kutoa huduma kwa wananchi.
Awali, wananchi wa
Wilaya ya Busega ambao husafiri takribani kilometa 130 kupata huduma za
kimahakama mjini Bariadi walimueleza Jaji Mfawidhi huyo adha wanayoipata
kutokana na kukosekana kwa huduma za Mahakama ya Wilaya Busega.
Mahakama ya Tanzania
inatekeleza ujenzi wa Mahakama za Wilaya mbalimbali kupitia Mpango wa Uboreshaji
wa Mahakama uliopo ndani ya Mpango Mkakati wa Mahakama (JSP) Awamu ya pili wa
mwaka 2020/2021 – 2024/2025 ambapo ujenzi wa Mahakama za Wilaya ya Itilima na
Busega ni sehemu ya mpango huo.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma (kulia)
akipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Itilima kutoka kwa
msimamizi wa mradi huo wakati alipotembelea mradi huo hivi karibuni.
Mtendaji wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Knyairita (kulia) akitoa maelezo ya mradi wa
ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu kwa Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma alipoembelea maendeleo ya
ujenzi wa Mahakama hiyo.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzanua, Kanda ya Shinyanga Mhe. Athuman Matuma (kushoto) akipata
maelezo ya mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Busega kutoka kwa Msimamizi
wa mradi huo wakati alipotembelea ujenzi wa Mahakama hiyo mwezi Machi, 2022.
Sehemu ya wananchi
kutoka Wilaya ya Busega waliofika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi kupata huduma
wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga
(hayupo katika picha) wakati alipotembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga (aliyesimama) akitoa
taarifa ya utendaji kazi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma wakati alipotembelea Mahakama hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya
Itilima, Mhe Faiza Salim akiongea jambo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma (hayupokatika picha) alipotembelea
jengo la Mahakama ya Wilaya ya Itilima linaloendelea na hatua za ujenzi.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athuman Matuma, (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Faiza Salim (wa
tatu kulia). Wengine ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe
Hussein Mushi, wa kwanza kulia, Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Bariadi Mhe.
Caroline Kiliwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Bi. Mavis Miti,
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu Bw. Gasto Kanyairita na Msaidizi wa
Sheria wa Jaji Mhe. Zawadi Ndudumizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni