Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe hivi karibuni
alikutana na viongozi mbalimbali wa dini mkoani hapo kujadili mambo kadhaa,
hususani suala la kuzingatia maadili katika jamii ili kupunguza ongezeko la
mashauri yanayofunguliwa mahakamani.
Katika kikao hicho
ambacho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe, Martin Shigela, viongozi hao
wameahidi kushirikiana na Mahakama kwa kuendelea kusisitiza waumini wao
kuzingatia maadili na kufuata sheria, hatua itakayosaidia kuwafanya waishi kwa
hofu ya Mungu.
Kikao hicho kimefanyika
kukutanisha uongozi wa Mahakama, wadau na viongozi wa dini mkoani hapa kwa
lengo la kutoa tathimini ya hali iliyopo katika Mahakama pamoja na
kuwashirikisha viongozi wa dini ili kufikia makundi mengi zaidi katika
kuwaelimisha wananchi juu ya sheria.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa kikao, Mhe. Ngwembe alisema kuwa Mahakama Morogoro inaamini kuwa
jamii ikipewa elimu ya kutosha juu ya masuala ya sheria itasaidia kupunguza
makosa mbalimbali yanayochangiwa na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu jambo
hilo.
Alisema kuwa idadi
kubwa ya waliopo magerezani ni waumini wa dini ya Kikristo au Kiislam na wa
chache ndio wapagani, hivyo kama elimu ya maadili na hofu ya Mungu itatolewa
katika nyumba za ibada itatoa mchango chanya katika kupunguza matukio
yanayoendelea kushika kasi ndani ya Mkoa wa Morogoro.
Mhe. Ngwembe alisema
takwimu mkoani Morogoro zinaonesha uwepo wa makosa ambayo yanajirudia rudia,
ikiwemo ubakaji wa watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18. Amesema kwa
mwaka 2021 mashauri 199 yameripotiwa, huku kwa mwaka 2022 kuanzia Januari hadi
Machi kuna mashauri 59 yameripotiwa.
Kwa mujibu ya Jaji
Mfawidhi huyo, ulawiti kwa mwaka 2021 kulikuwepo na mashauri 32 na mwaka 2022
kuanzia Januari hadi Machi kuna mashauri matano ambayo tayari yamelipotiwa.
Ametaja makosa mengine
kama dawa za kulevya ambapo kwa mwaka 2021 kulikuwepo na mashauri 188 na mwaka
2022 kuanzia Januari mpaka March kuna mashauri 52 ambayo tayari yameshalipotiwa. Kosa lingine ni kukamatwa
na nyara za serikali ambazo kwa mwaka 2021 kulikuwepo na mashauri 53 na kwa
mwaka 2022 kuanzia Januari mpaka Machi kuna mashauri 42.
Kuhusu mauaji, Mhe.
Ngwembe amesema kuwa kwa mwaka 2021 kulikuwepo na mashauri 95 na kwa mwaka 2022
kuanzia Januari hadi Machi kuna mashauri 26 ambayo tayari yameripotiwa
mahakamani.
Alibainisha kuwa miongoni mwa kundi kubwa la
mahabusu na wafungwa waliopo katika magereza ya Mkoa huo ni vijana wenye umri
chini ya miaka 35, hali ambayo ni hatari kwa taifa, kwani kundi hilo ndio lenye
nguvu ya kufanya shuguli za uzalishaji.’
Aidha, Mhe. Ngwembe
alikemea tabia ya jamii ya kuwaficha wahalifu, huku akitolea mfano kuwa kilimo
cha dawa za kulevya aina ya bangi kinafanyika hadharani na jamii inaona na
kukaa kimya badala ya kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Akichangia mazungumzo
hayo, Mchungaji Sauli Kajula kutoka Kanisa la Moraviani alishauri elimu ya dini
mashuleni iwe somo la lazima kama yalivyo masomo mengine na kuahidi kuwa wao
kama viongozi wa dini watawalea vijana katika dhamira njema na matumaini yao ni
kuhakikisha matukio ya ukosefu wa maadili yanapungua kama sio kumalizika
kabisa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro aliishukuru Mahakama kwa kuweka bayana masuala mbalimbali
yanayojitokea katika jamii na kuahidi kuwa yote yaliyosemwa wameyapokea kama
serikali na ameahidi kutoa ushirikiano.
Mhe. Shigela aliwaomba
viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kukaa katika misingi inayokubalika kiimani
ili kupunguza makosa yanayojitokeza ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na
jamii kukosa hofu ya Mungu.
Mahakama ya Tanzania
Mkoa wa Morogoro imekuwa na utaratibu wa kuwafikia wananchi ili kuwapa elimu ya
sheria kuhakikisha wanapunguza mashauri yanayojirudia mara kwa mara.
Awali, elimu hiyo
ilikuwa ikitolewa upitia vyombo vya habari mkoani humo kuanzia Novemba 2021 na
baadae ilianza kutolewa kwa wananchi wanaofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki na takwimu zinaonyesha tangu huduma hiyo ianze kutolewa mwezi machi 2022,
wananchi takribani 2,723 wamenufaika na elimu hiyo.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (mwenye tai
nyekundue) akiongoza msafara baada ya zoezi la upandaji miti.
Kamati ya Ulinzi na Usalama
Mkoa wa Morogoro wakifuatilia mjadala wakati wa kikao kilichoandaliwa na
Mahakama na kuwashirikisha wadau na viongozi wa dini mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Mhe Martin Shigela akipanda mti wa matunda katika eneo la Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoani Morogoro baada ya kikao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni