Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania leo tarehe 1 Mei, 2022 imeungana na
Watanzania kote nchini kusherekea siku ya wafanyakazi duniani, maarufu kama Mei
Mosi.
Sherehe hizo ambazo zimefanyika kitaifa jijini Dodoma ambayo ni
Makao Makuu ya Tanzania zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali, hususani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Mpango na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa.
Kwenye orodha hiyo alikuwepo pia Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ambapo Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwakilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe Dkt Adam Mambi.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa Jamhuri
jijini hapa, Rais Samia ameahidi kuimarisha
maslahi ya wafanyakazi nchini.
Amesema kwa kuwa alishatoa ahadi mwaka jana kuhusu suala hilo
ameagiza kufanyika kwa majadiliano ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kati ya
Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA) na Serikali ili kujua kiwango
kinachohitajika.
“Ninakubaliana nanyi kabisa kwamba viwango vya sasa vya mshahara
havikidhi mahitaji ya mfanyakazi pamoja na familia yake, hususani nyakati kama
hizi ambapo gharama za maisha zimepanda,” alisema Mhe. Samia.
Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Serikali imeshaunda bodi za
kima cha chini cha mshahara kwa sekta zote na tayari zimeanza kufanya tathmini
ili kufanya uboreshaji wa kima cha chini cha mshahara kilichopo sasa, hivyo
ameziagiza Wizara zinazohusika kuhakikisha bodi zinawezeshwa ili kufanikisha
jambo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni