Ijumaa, 29 Aprili 2022

JAJI MKUU ATETA NA MKURUGENZI ILO; AIOMBA KUWEKEZA MATUMIZI YA MTANDAO

Na Magreth Kinabo – Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  ameliomba Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuendelea kuiwezesha Mahakama hususani Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi ili iweze kujiendesha kimtandao.

Akizungumza leo tarehe 29 Aprili, 2022 na ujumbe wa Shirika hilo uliongozwa na Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe, Jaji Mkuu amesema Dunia sasa inakwenda kidijitali/kimtandao, hivyo ni vizuri kuwekeza katika suala hilo.

‘‘Vilevile ni vema Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ikawezeshwa ili iweze kufanya kazi zake kimtandao, kwa kuwa itasadia kutoa haki,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza kuwa ni vizuri pia suala la Usuluhishi wa Migogoro kwa njia Mbadala (ADR) ikafanyika kwa njia ya kimtandao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ILO, Bw. Chibebe amesema kuwa, Shirika hilo limeendelea kufanya kazi kwa pamoja na Divisheni ya kazi kupitia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi hususani kwenye utoaji wa Mafunzo ya aina mbalimbali yanayolenga kuwezesha uendeshaji fasaha wa mashauri yanayohusu masuala ya kazi ili wafanyakazi waweze kupata haki zao na kutatua changamoto zilizopo.

‘‘Tutaendelea kusaidia Mahakama kwenye maeneo ya mashauri ya kazi, kujenga uwezo, kutoa mafunzo na maeneo mengine,’amesema Chibebe.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amesema ILO imekuwa ikiwasaidia kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama ya Kazi, kutoa mafunzo kuhusu Sheria za Kazi nchini zikiwemo za viwango vya kimataifa kwa Majaji, Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi Wafawidhi.

Aliongeza kwamba ILO imesaidia kutoa mafunzo watumishi wengine wa Mahakama hiyo katika maeneo ya maadili, jinsi ya kutoa huduma kwa mteja na kadhalika.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe wakizungumza wakati Mkurugenzi huyo na Ujumbe alioambatana nao walipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam leo tarehe 29 Aprili, 2022.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza jambo katika kikao baina yake na Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe na ujumbe alioambatana naye.

Kikao kikiendelea kati ya Mahakama ya Tanzania na Ujumbe kutoka 'ILO'.

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe akizungumza na Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma (hayupo katika picha).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza jambo katika kikao hicho.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na  Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na  Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu- Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi.

Picha ya pamoja: Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kushoto ni
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu- Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi. Wa kwanza kulia ni  Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wellington Chibebe na sehemu ya Maafisa wa Shirika hilo walioambatana na Mkurugenzi huyo.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni