Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Mashindano ya Mei Mosi yaliyokuwa yanafanyika katika Uwanja wa
Jamhuri jijini hapa yamekamilika leo tarehe 29 Aprili, 2022 kwa timu ya
Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) kushika nafasi ya pili kwenye mchezo wa
kuvuta kamba wanaume na wanawake.
Mahakama Sports iliingia fainali kupambana na timu ya Uchukuzi kwa
upande wa wanaume na wanawake, lakini ikashindwa kwa taabu na wapinzani wao,
hivyo kuweza kujinyakulia vikombe viwili baada ya kushika nafasi ya pili.
Ilikuwa mchezo wa kamba wanawake ulioanza majira ya mchana huku timu
zote mbili zikikamiana. Katika mzunguko wa kwanza, timu ya Uchukuzi ilifanikiwa
kupata pointi moja baada ya kuwazidi ujanja Mahakama Sports. Hata hivyo,
Mahakama Sports walikuja juu katika mzunguko wa pili na kufanikiwa kuwaburuta
Uchukuzi, hivyo ngoma ikabaki sawia kwa pande zote mbili.
Waamuzi walilazimika kuchezesha mzunguko wa pili ili kuweza kupata
mshindi, ndipo Uchukuzi walipofanikiwa kupata pointi nyingine ya pili baada ya
Mahakama Sports kuteleza wakati wakiwa wamebakiza upenyo mchache kushinda,
hivyo kuwawezesha wapinzani wao kutumia faida hiyo na kuibuka washindi.
Mchezo wa wanaume haukuwa mgumu, ila ulitawaliwa na ujanja kwa upande
mmoja. Katika mizunguko yote miwili, Uchukuzi walitumia ujanja wa kuachia kamba
kabla ya mwamuzi kupuliza filimbi, hatua iliyowafanya Mahakama Sports kulegeza.
Kitendo hicho kiliwafanya Uchukuzi kuvuta kamba kwa nguvu na kwa
kushitukiza, huku Mahakama Sports wakiwa bado hawajajiandaa, hivyo kuwafanya
wapinzani hao kujipatia pointi zote mbili zilizowawezesha kuibuka washindi.
Akizungumza baada ya fainali hizo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports
Wilson Dede amewashukuru wachezaji wote kwa mafanikio makubwa licha ya timu
pinzani kufika kwenye michuano hiyo kwa kuikamia Mahakama.
“Timu zote katika mashindano haya zilikuwa zinaiangalia Mahakama
kwa sababu wanatujua vilivyo. Hata hawa waliobahatika wanatujua sisi ni nani,
leo wamebahatisha ndiyo maana wameshangilia uwanja mzima kwa sababu walikuwa
wanapambana na mwamba. Tunajipanga kwa mashindano yajayo,” amesema.
Kwa upande wake, Mwalimu Spear Mbwembwe amewapongeza vijana wake kwa
kazi nzuri na kujituma sio tu kwenye mazoezi lakini hata wanapokuwa kwenye
mapambano uwanjani. “Sisi ni washindi, wala hatujapoteza. Kuna timu 41
zilizokuwepo hapa, lakini sisi tumekuwa wa pili. Lazima tujipongeze,” amesema.
Ushindi huo umeshuhudiwa na Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso, ambaye pia ni mlezi wa Timu hiyo na Mkurugenzi
wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick, ambao wote kwa pamoja
wamewapongeza wachezaji kwa kuiheshimisha Mahakama. Wameahidi kuwapa
ushirikiano ili waweze kufanya vizuri zaidi kwanye mashindano yajayo.
Mashujaa hao wa Mahakama Sports wanawake walioshiriki katika
mashindano hayo wakiongozwa na mama Mchawi Mwanansolo walikuwa Stephania
Bishobe, Zahara Selemani, Rebecca Mwakabuba, Hadija Mkuvi, Beatrice Dibogo,
Jamila Kisusu, Judith Sarakikya, Saraphina Mkumbo, Melina Mwinuka, Namweta
Mcharo, Mwanabibi Bakari, Lucy Mbwaga, Zuhura Hamza, Scholastica Shemtoi na
Josephine Aidani.
Kwa upande wa Mahakama Sports wanaume chini ya Rajab
Mwariko walikuwa Leonard Kazimzuri, Cletus Yuda, Seleman Dimoso, Patrick
Nundwe, Denis Chipeta, Frank Lutego, Ashel Chaula, Abdul Mbaraka, Mushi Martin,
Moris Magogo, Chilemba Chikawe, Issa Kabandika, Philipo Ferdinand, Emmanuel
Seshahu na Fred Ndimbo.
Mahakama Sports iliingia robo fainali baada ya kushinda mechi zake
zote kwenye hatua ya makundi. Mahakama Sports wanaume walimenyana na TPDC na
Tanesco, ambao waliingia mitini kwa kuhofia kipigo, huku Mahakama Sports
wanawake ikiwazalisha Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Baada ya
hapo, Mahakama Sports ilikutana na TPDC kwenye nusu fainali na kufanikiwa
kutinga fainali kukutana na Uchukuzi.
Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao waliambatana na
Mahakama Sports ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende,
Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi
Mwanansolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na
Meneja Vifaa na Tiba Teresia Mogani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni