Alhamisi, 28 Aprili 2022

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA AWAITA WANANCHI KWENYE KITUO HUDUMA MASAA 24

 Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewaomba wananchi kuendelea kutumia kituo maalumu kilichoanzishwa na Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma zitolewazo, malalamiko na mapendekezo kwa wadau mbalimbali wa haki nchini.

Prof. Ole Gabriel ametoa rai hiyo leo tarehe 28 Aprili, 2022 alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari katika viunga vya Bunge jijini hapa mara baada ya kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa na Waziri, Mhe. Dkt Damas Ndumbaro.

“Kituo hicho kinachofanya kazi kwa masaa 24 kila siku kina malengo makubwa matatu, kufungua uwigo wa kujua jinsi gani ambavyo wadau wetu wamepokea huduma zetu kwa sababu kwenye huduma kuna kuridhika na pia kuna kutokuridhia, kuhakikisha kwamba tunakuwa na uwezo wa kupata maoni  na ushauri wa wadau wetu na pia sisi kuboresha huduma zetu ziendane na mahitaji ya Mahakama,” amesema.

Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama amebainisha kuwa ndani ya Mahakama kuna mageuzi makubwa ya utoaji ya huduma na kwamba kuna mambo matatu yanayozingatiwa katika utoaji wa haki ambayo ni uwazi, ubora wa huduma na ufikaji wa huduma hizo kwa wananchi kwa njia rahisi zaidi.

“Kwa sasa kituo hiki kina watumishi takribani 12 na kati yao sita ni watumishi wanaoshughulikia masuala ya kiutawala zaidi na rasilimali watu na wengine wataalamu wa masuala ya kisheria. Kwenye kituo hiki tumeweka wasimamizi ili wale wanaohusika waweze kufanya kazi kama timu,” amesema.

Prof. Ole Gabriel alizitaja baadhi ya huduma ambazo wananchi wanaweza kuzipata kutoka kwenye kituo hicho kama kuulizia masuala ya utaratibu wa jambo lolote linalohusu upatikanaji wa huduma za kimahakama ikiwemo masuala ya mirathi na ndoa na kupokea mrejesho wa jinsi huduma zinavyokidhi matarajio ya mteja.

Amezitaja huduma zingine kama wananchi kutoa malalamiko kuhusu jambo mahsusi  ambalo kiutawala mteja hajaridhika nalo na angependa kufahamu uratatibu wa kulishughulikia, kutoa taarifa ya vitendo vyovyote vinavyosababisha ukiukwaji wa kimaadili katika mnyororo wa utoaji huduma ndani ya Mahakama na kutoa ushauri wowote wa jinsi ya kuboresha huduma za Mahakama.

Aidha, Mtendaji Mkuu huyo aliwaambiwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa huduma hiyo itafikishwa pia kwa wafungwa na mahabusu ili nao waweze kuwasilisha dukuduku zao katika kituo hicho kwa njia ya maandishi wakiwa katika maeneo yao.

“Naomba wananchi wafahamu kuwa mpango huu sio mbadala wa rufani wala sio njia ya kupingana na uamuzi halali wa kisheria bali ni utaratibu wa kiutawala wa kuhakikisha kuwa haki inazidi kutendeka kwa uwazi na mteja aridhike kuwa haki yake haijacheleweshwa wala kufichwa kwa namna yoyoye,” Prof. Ole Gabriel alisema.

Amewaomba wananchi ndani na nje ya Tanzania kuwasilisha taarifa au dukuduku zao kwenye kituo hicho kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa kawaida au WhatsApp kwenye namba ya kituo ambayo ni 0752500400 au kwa njia ya barua pepe (email); maoni@judiciary.go.tz.

Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel, njia nyingine ni kupakua  mfumo wa mrejesho kwenye simu njanja ya mteja kwenye ‘google store’ kwa kupakua Judiciary Mobile TZ, kisha kitufe cha Mrejesho, unajaza maswali machache yaliyopo kwenye mfumo huo na kubofya kitufe cha kutuma. Njia nyingine ni kutumia tovuti ya Mahakama ambayo ni www.judiciary.go.tz.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu matumizi ya kituo maalumu cha huduma masaa 24 kilichoanzishwa na Mahakama ya Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiingia katika viunga vya Bunge.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) akifuatilia mjadala Bungeni akiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe, Wilbert Chuma (kushoto).





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni