Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Wabunge wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji mkubwa wa
huduma za utoaji haki, ikiwemo mindombinu ya majengo, matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuanzisha kituo kwa lengo la kupata mrejesho
wa huduma zitolewazo, malalamiko na mapendekezo.
Miongoni mwa Wabunge
hao, Mhe. Asha Abdalla, Mhe. Joseph Tadayo, Augusta Rambati na Mhe.
Issa Mtemvu wametoa pongezi hizo leo
tarehe 28 Aprili, 2022 walipokuwa wakichangia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria,
Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na
matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Tunaipongeza sana
Mahakama kwa kazi nzuri inayofanya, ikiwemo uboreshaji wa huduma za utoaji
mbalimbali za haki kwa wananchi na ujenzi wa majengo ya kisasa. Mimi ni Mjumbe
wa Kamati ya Sheria na Katiba. Tumetembelea baadhi ya miradi ya majengo, kwa
kweli tumeiona thamani ya fedha katika majengo hayo,” Mhe. Asha Abdalla
alisema.
Akichangia hotuba hiyo,
Mhe. Augusta Rambati, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria
alianza kwa kumpongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika kusimamia shughuli
mbalimbali za kiutendaji ndani ya Mhimili huo wa dola.
“Nimeshiriki katika
ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyopo chini ya Mahakama. Nikiri kwamba
kwa macho yangu nimeona thamani ya fedha. Nichukue fursa hii kuwapongeza kuwa
fedha ambazo zimetengwa hakika Mahakama wamezitendea haki na thamani ya fedha inaonekana
kabisa,” amesema.
Kwa upande wake, Mhe.
Tadayo alieleza kuwa alipata fursa ya kutembea na Kamati ya Katiba na Sheria kuangalia
miradi mbalimbali ya maendeleo ya
Mahakama ambayo ipo chini ya Wizara hiyo na amekiri kuona maendeleo makubwa
katika uboreshaji wa sekta ya utoaji haki kwa wananchi.
“Tumeona majengo ya
kisasa, uboreshaji mkubwa wa mifumo ya TEHAMA pamoja na hiki kituo ambacho kinawasaidia wananchi kupeleka kero zao. Pia tumeona ushirikishwaji wa wadau
wengine,” amesema.
Mhe. Tadayo alitoa mfano
wa kitendo cha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupewa ofisi ndani ya jengo
la Mahakama ili watu wote wanaohitaji msaada wa kisheria waweze kupata katika
eneo moja. Amesema kitendo hicho ni mapinduzi makubwa yanayodhihirisha kuwa
Serikali haifanyi maigizo kwenye suala zima la utoaji haki.
Awali akiwasilisha makadirio
ya mapato na matumizi ya Wizara yake, Mhe. Dkt Ndumbaro aliliambia Bunge kuwa Mahakama
imeendelea na utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) wa
Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama, ambapo katika mwaka 2021/2022
miradi 37 ilitekelezwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
Amesema kuwa hadi kufikia
Machi, 2022 miradi imefikia katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwemo ujenzi
wa vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) sita katika Mikoa ya Dar es salaam
(Kinondoni na Temeke), Dodoma, Morogoro, Mwanza na Arusha.
Kumekuwepo pia na ujenzi
wa Mahakama za Hakimu Mkazi mbili katika Mikoa ya Katavi na Lindi; ujenzi wa
Mahakama za Wilaya nne katika Wilaya za Bahi, Chemba, Rungwe na Bunda; ujenzi
wa Mahakama za mwanzo tatu za Matiri (Mbinga), Hydom (Mbulu) na Kibaigwa
(Kongwa) na ujenzi wa Jengo la Kuhifadhia Kumbukumbu – Tanga.
Waziri Ndumbaro ametaja
miradi inayoendelea kama ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama Dodoma
ambapo ujenzi wa boma umekamilika kwa asilimia 100; ukarabati na upanuzi wa
Mahakama Kuu Tabora na ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi katika Mikoa ya
Songwe na Tabora.
Pia kuna ujenzi wa
Mahakama za Wilaya za Nanyumbu, Namtumbo, Same, Tandahimba, Kilindi, Sikonge,
Mwanga, Kakonko, Buhigwe, Uvinza, Butiama, Rorya, Itilima, Busega, Songwe,
Mbogwe, Nyang’wale, Kyerwa, Misenyi, Gairo, Mvomero, Kilombero, Mkinga,
Tanganyika na Kaliua.
Ametaja miradi mingine
inayoendelea ambayo ni ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Mang’ula na Mlimba
(Morogoro), Nyakibimbili (Bukoba), Kabanga (Ngara), Chanika (DSM), na Kimbe
(Kilindi) na Ujenzi wa bweni la wavulana katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama -
Lushoto.
Mhe. Dkt Ndumbaro
amebainisha pia kuwa Mahakama imeendelea kuanzisha na kuboresha mifumo ya
utoaji haki kwa kutumia TEHAMA na hadi kufikia Machi 2022, Mahakama imeanzisha
mfumo wa ‘SEMA NA MAHAKAMA’ wenye lengo la kupata mrejesho wa huduma
zitolewazo, malalamiko na mapendekezo.
Kwa mujibu wa Waziri
Ndumbaro, vilevile Mahakama imefanya uboreshaji katika mifumo mbalimbali,
ikiwemo mfumo wa kielektroniki wa usimamizi na uendeshaji wa mashauri (Judicial
Statistical Dashboard System - JSDS II) na mfumo wa Mkutano Mtandao (Video
Conferencing) unaowezesha kuendesha mashauri kwa njia ya mtandao.
Pia kuna mfumo wa
kielektroniki wa kusajili na kuwatambua mawakili (eWakili); mfumo wa kutambua
Viwanja na Majengo ya Mahakama (JMap) wenye lengo la kutambua hali halisi ya
majengo na viwanja vya Mahakama ili kuwezesha uandaaji wa mpango wa ujenzi na
ukarabati wa majengo ya Mahakama nchi nzima na mfumo wa kuratibu na kuhifadhi
taarifa za mali na vitendea kazi mahakamani.
Akiwasilisha maoni ya
Kamati kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Mfuko wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2021/22
pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23, Mjumbe wa
Kamati ya Katiba na Sheria, Mhe. Issa Mtemvu alivitaja baadhi ya vipaumbele vya
Mahakama katika mwaka wa fedha 2021/22.
Vipaumbele hivyo ilikuwa
kuboresha mifumo ya TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma; kuongeza
ushirikiano na wadau wa haki jinai ili kuharakisha huduma ya utoaji haki na kuendelea
kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi
mbalimbali nchini.
Amesema mafanikio
yaliyofikiwa katika kutekeleza vipaumbele hivyo ni kuboresha mfumo wa
teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kama nyezo muhimu ya kuboresha
utoaji wa huduma na kuendelea kutekeleza mpango (2021/22 – 2025/26) wa ujenzi
na ukarabati wa mahakama katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji
wa miradi 37 katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. George Masaju akipokea salamu kutoka kwa Wabunge wakati wa utambulisho
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Tulia Ackson akisistiza jambo kabla ya Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe. Dkt Ndumbaro kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake Bungeni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni