· Yatinga fainali kwa mkwara baada ya kuwakaangiza TPDC
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 27
April, 2022 imetinga fainali kwenye mchezo wa kuvuta kamba wanaume na wanawake katika
mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa baada
ya kuwapa kipigo kitakatifu TPDC.
Mashindano yaliyozikutanisha timu hizo yalianza majira ya saa moja
asubuhi, ambapo TPDC walionekana kuukamia mchezo huku wakihamasishana ili kulisabaratisha
Jabali la Mahakama. Hata hivyo juhudi zao hazikuzaa matunda mara baada ya kuangukia
pua na kujikaanga kwenye mafuta yao wenyewe.
Ilikuwa Mahakama Sports wanawake waliokuwa wa kwanza kuingia
katika mchezo dhidi ya TPDC wanawake ambao ulionekana kuwa mgumu, huku timu
zote mbili zikisomana mbinu za uchezaji. Hatimaye Mahakama Sports walifanikiwa
kuwango’a wapinzani wao kwenye mzunguko huo.
Mzunguko wa pili haukuwa rahisi kwa timu zote mbili ambapo Mahakama
Sports walionyesha ubabe walionao dhidi ya wapinzani wao. Hata hivyo, TPDC walifanikiwa
kuchomoza baada ya Mahakama Sports kutereza na kudondoka, hivyo kuwapa nafasi
wapinzani wao kuvuta kamba haraka haraka na kupata pointi moja.
Iliwalazimu waamuzi kuchezesha mzunguko wa tatu ili kupata
mshindi. Mahakama Sports walitulia, wakajipanga na kwa kutumia mbinu za
kimchezo walizokuwa wamefundishwa na Mwalimu Spear Mbwembwe walicharuka kama
nyuki na wakafanikiwa kuwakaanga TPDC, ambao hawakuamini macho yao.
Mchezo wa wanaume ulianza kwa ushindani mkubwa huku TPDC wakiwa na
kumbukumbu ya kupoteza mchezo walipokutana na Mahakama Sports wanaume wakati wa
makundi. Hivyo, TPDC walikamia mchezo huo kwa nia ya kulipiza kisasi.
Hata hivyo, usemi wa Wahenga kuwa Jabali ni Jabali tu uliendelea
kujidhihirisha baada ya TPDC kutolewa kamasi na Mahakama Sports wanaume katika mizunguko
yote miwili. Ingawa TPDC walijaribu kujitutumua kwa kubadilisha mbinu za uchezaji,
juhudi hizo ziligonga mwamba na kuliacha Jabali likiondoka na kamba, huku wao
wakiangukia pua bila kitegemea.
Baada ya kumalizika kwa michezo hiyo miwili, Mwenyekiti wa
Mahakama Sports Wilson Dede amewashukuru kwa mara nyingine tena wachezaji wote
kwa mafanikio makubwa ambayo wameyafikia hadi sasa, hususani kufika fainali
katika mchezo huo.
“Ingawa
wenzetu walikuwa wametukamia, lakini tumewaonyesha sisi ni nani. Sasa tuna kazi
moja tu, nayo nikutembeza vichapo na kubeba makombe yote. Uwezo huo tunao, nia tunayo,
twendeni tukamalizie kazi iliyotuleta. Sisi ni Jabali ambalo limeshindikana na halitikisiki,”
alisema.
Kwa upande wake, Mwalimu Mbwembwe amewakumbusha
vijana wake kuwa hawana kitu kingine zaidi ya kuzoa makombe yote katika mchezo
huo. “Wembe ni ule ule, wameutaka wenyewe na wanataka kuuchezea, lazima uwakate,
watake wasitake,” alisema.
Baadaye, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango
wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso, ambaye pia ni mlezi wa Timu hiyo,
alitembelea kambi ya Mahakama Sports ambapo amewapongeza wanamichezo wote kwa
kuendelea kuiheshimisha Mahakama kwa kufanya vizuri katika mashindano
mbalimbali.
“Nizipongeze timu zote mbili kwa ushindi
huu mlioupata leo. Nimewaona uwanjani mlivyokuwa mnapambana. Ingawa mchezo wa kamba ni kama dakika tano hivi, lakini shughuli
yake ni zaidi ya dakika 90. Mmefanya kazi kubwa na hongereni sana. Nizidi
kuwatia moyo, tumalizie huu ushindi,” alisema.
Mkurugenzi huyo pia aliwafikishia
wachezaji hao salamu kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel ambaye ametoa pongezi za dhati kwa mafanikio waliyoyapata
na anafuatilia kwa karibu mashindano hayo.
“Kama mlivyoanza mwanzo, endeleeni na jitihada hizo hizo, tumalize vizuri, tuondoke na ushindi na tukawakabidhi viongozi wetu vikombe. Nina uhakika tutachukua makombe yote,” alisema. Kwa upande wao, wachezaji wa timu zote mbili wamemhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa watapambana kwa nguvu zao zote ili kuibuka washindi.
Kikosi kilichoanza kwa upande wa Mahakama Sports wanawake wakiongozwa na mama Mchawi Mwanansolo kilihusisha Stephania Bishobe, Zahara Selemani, Rebecca Mwakabuba, Hadija Mkuvi, Beatrice Dibogo, Jamila Kisusu, Judith Sarakikya, Saraphina Mkumbo, Melina Mwinuka na Namweta Mcharo. Waliokaa benchi walikuwa Mwanabibi Bakari, Lucy Mbwaga, Zuhura Hamza, Scholastica Shemtoi na Josephine Aidani.
Walioanza kwa upande wa
Mahakama Sports wanaume chini ya Rajab Mwariko walikuwa Leonard
Kazimzuri, Cletus Yuda, Seleman Dimoso, Patrick Nundwe, Denis Chipeta, Frank
Lutego, Ashel Chaula, Abdul Mbaraka, Mushi Martin na Moris Magogo. Waliokaa
benchi walikuwa Chilemba Chikawe, Issa Kabandika, Philipo Ferdinand, Emmanuel
Seshahu na Fred Ndimbo.
Michezo mingine ya nusu fainali kwa
upande wa wanawake iliwakutanisha Uchukuzi ambao waliwatoa kwenye mashindano Tamisemi.
Kwa upande wa wanaume, Uchukuzi pia waliwapigisha kwata Mambo ya Ndani. Kwa
maana hiyo, Mahakama Sports itakutana na Uchukuzi kwenye fainali.
Mahakama Sports iliingia robo fainali baada ya kushinda mechi zake
zote kwenye hatua ya makundi. Mahakama Sports wanaume walimenyana na TPDC na
Tanesco, ambao waliingia mitini kwa kuhofia kipigo, huku Mahakama Sports
wanawake ikiwatambia Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana na
Mahakama Sports ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende,
Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi
Mwanansolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na
Meneja Vifaa na Tiba Teresia Mogani.
Mahakama Sports wanawake wakilia kwa furaha baada ya kuwakaanga TPDC wanawake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni