Jumanne, 26 Aprili 2022

MAHAKAMA SPORTS MTU NA NUSU

·Yatinga Nusu Fainali kibabe

· Yatibua Mipango na kuisasambua Kilimo

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 26 April, 2022 imetinga nusu fainali kwenye mchezo wa kuvuta kamba wanaume na wanawake katika mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa baada ya kuwaadhibu vikali wapinzani wao, timu za Mipango na Kilimo.

Ilikuwa Mahakama Sports wanawake waliokuwa wa kwanza kuingia katika mchezo dhidi ya Kilimo ambao ulianza majira ya saa moja asubuhi ambapo katika mzunguko wa kwanza wapinzani hao walijaribu kutoa upinzani, lakini wakakumbana na kipigo kikali, hivyo kuachia pointi muhimu kwa Mahakama.

Kazi ilikuwa nyepesi katika mzunguko wa pili ambapo Mahakama Sports walionekana dhahiri kuwazidi mbinu na ujanja wa kimchezo washindani wao mara baada ya kuwafurusha mara moja na kuwaonyesha kuwa Kilimo ni sawa na mboga ya mlenda, hivyo kuwaacha wakigalagala chini pasipokuwa na msaada wowote.

Mchezo wa Mahakama Sports wanaume ulianza kwa ushindani mkubwa ambapo Mipango waliingia uwanjani wakiwa na mipango madhubuti ya kutoka na ushindi. Hata hivyo, Mahakama ilithihirisha umwamba wake mara baada ya kutibua mipango ya washindani wao na kuwaacha wakilaumiana.

Katika mzunguko wa kwanza na wa pili, haikuchukua muda kwa Mahakama Sports kuwaonyesha Mipango kuwa wapinzani hao si lolote wala chochote walipoangukia pua mara mbili na kuwaacha washindi hao wakijizolea pointi zote mbili zilizowavusha katika hatua ya nusu fainali.

Kufuatia hatua hiyo, Mahakama Sports wanawake watakabiliana na TPDC katika hatua ya nusu fainali itakayochezwa kesho tarehe 27 Aprili, 2022, huku Mahakama Sports wanaume wakionyeshana umwamba kwa mara nyingine na TPDC. Katika hatua ya makundi, timu hizi zilikutana na TPDC wakachakazwa vikali.

Akiongea mara baada ya mchezo huo kumalizika, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewashukuru wachezaji wote kwa moyo wa kujituma na kuendelea kufanya vizuri katika mashindano hayo. Amewashukuru pia kwa kuzingatia maelekezo ya mwalimu, lakini hakusita kuwaonya wapinzani wao.

“Labda niwakumbushe wapinzani wetu kuwa sisi ni Dude Kuuubwa! Mahakama Sports ni Mtu na Nusu! Naomba wasijisahaulishe hilo, na kipigo kitaendelea kwa yoyote atakayejaribu kututunishia misuri. Sisi tunapenda kutoa haki, na haki ndiyo hii, au wewe unaonaje,” Dede alimuuliza Mwandishi wa habari hizi.

Kwa upande wake, Mwalimu Spear Mbwembwe amewapongeza vijana wake kwa kuwa na ari ya mchezo, kucheza kitimu na kuzingatia yote aliyokuwa amewaelekeza ili kupata ushindi. “Nataka nikwambie mambo mazuri yanakuja. Sitaki kusema mengi, lakini yule anayefuata atapata kichapo kitakatifu zaidi,” alisema.

Kikosi kilichoanza kwa upande wa Mahakama Sports wanawake wakiongozwa na mama Mchawi Mwanansolo kilihusisha Hadija Mkuvi, Zahara Abdalla, Stephania Bishobe, Jamila Kisusu, Rebecca Mwakabura, Sarafina Mkumbo, Judith Sarakikya, Beatrice Dibogo, Mwanabibi Bakari na Namweta Mcharo. Waliokaa benchi walikuwa Zuhura Abdallah, Lucy Mbwaga, Melina Mwimika, Scholastica Shemtoi na Josephine Aidani.

Walioanza kwa upande wa Mahakama Sports wanaume chini ya Rajab Mwariko walikuwa Leonard Kazimzuri, Cletus Yuda, Seleman Dimoso, Patrick Nundwe, Denis Chipeta, Frank Lutego, Philipo Ferdinand, Ashel Chaula. Mushi Martin na Moris Majogo. Waliokaa benchi walikuwa Chilemba Chikawe, Issa Kabandika, Fred Ndimbo, Abdul Mbaraka na Magessa Mgeta.

Mechi zingine zilizochezwa katika hatua hiyo ya robo fainali kwa upande wa wanaume ni Uchukuzi walioibuka washindi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kilimo walioangukiwa pua kwa TPDC na Ngorongoro waliopigishwa kwata na Mambo ya Ndani.

Kwa upande wa wanawake robo fainali, Tamisemi waliibuka wababe wa Ocean Road, TPDC wakawaadhibu Ngorongoro, ambapo Uchukuzi ‘wakachota fedha’ za Hazina na kuwafanya wayaage mashindano.

Mahakama Sports iliingia robo fainali baada ya kushinda mechi zake zote kwenye hatua ya makundi. Mahakama Sports wanaume walimenyana na TPDC na Tanesco, ambao waliingia mitini kwa kuhofia kipigo, huku Mahakama Sports wanawake ikiwatambia Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana na Mahakama Sports ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanansolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa na Tiba Teresia Mogani.

Mwamuzi katika mchezo wa kamba akipuliza kipenga kuashiria ushindi wa Mahakama Sports wanawake ambao waliwafanyia kitu mbaya timu ya Kilimo na kutinga nusu fainali kwenye mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mahakama Sports wanawake wakiwakamua wapinzani wao Kilimo.

Mahakama Sports wanaume (picha ya juu) wakitoa kipigo kikali kwa timu ya Mipango (picha ya chini) na kuwaacha wakigalagala chini bila msaada wowote.

Mahakama Sports wanawake wakishangilia mara baada ya kuwasambaratisha Kilimo.

Mahakama Sports wanaume wakikatisha kwenye Uwanja wa Jamhuri kibabe baada ya kutoa kipigo kikali na kutibua Mipango.


Timu ya Mahakama Sports wakishangilia wakiwa jukwaani mara baada ya kutembeza vipigo kwa timu pinzani.
Ni raha iliyoje- sehemu ya Mahakama Sports wanawake wakianikiza furaha kwa matarumbeta baada ya kuifumua Mipango na Kilimo.
Timu ya TPDC wanawake wakishangilia mara baada ya kuwafurusha kwenye mashindano timu ya Ngorongoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni