Na Francisca Swai, Mahakama-Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewataka watumishi wa Kanda hiyo kuungana kwa pamoja na kusaidia kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka (2020/2021-2024/2025) ili Mhimili huo uweze kufikia malengo yake kwa ufanisi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo hivi karibuni, Mhe. Mtulya alisema kuwa ili kufikia malengo ya kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo ni muhimu Watumishi kushirikiana na kufanya shughuli zote kwa upendo.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya alipata fursa ya kuuelezea mpango mkakati huo na kuwaeleza watumishi kuwa mpango huo utashushwa kwa kila ngazi ya Mahakama ili waweze kuwafanya kazi katika njia moja na hatimaye kuifikia azma ya Mahakama ya kutoa haki kwa wakati.
Katika kikao hicho kilichowashirikisha watumishi wote wa Mahakama katika kila ngazi ilisisitizwa umuhimu wa kila Mtumishi kuujua mpango mkakati wa Mahakama 2020/21-2024/25 kwa urahisi wa utekelezaji wake.
Katika mkutano wa Baraza hilo wajumbe waliafikiana jumla ya maazimio nane ikiwemo watumishi wote wa Mahakama kuwekwa kwenye mfumo mmoja wa malipo ya mshahara yaani ‘TJS’, watumishi waliojiendeleza nje ya kada zao kufikiriwa kubadilishwa kada, watumishi waliosahaulika kupandishwa cheo waombewe kibali maalumu cha kupandishwa cheo na kadhalika.
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya akiuelezea Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/21-2024/25 kwa wajumbe wa Baraza hilo (hawapo katika picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni