Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 25
April, 2022 imeendelea kufanya mazoezi muhimu kabla ya kukutana robo fainali na
timu za Mipango na Kilimo katika mchezo wa kuvuta kamba wanaume na wanawake kwenye
mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na viongozi wa mashindano hayo, mechi
za robo fainali zitachezwa kesho tarehe 26 Aprili, 2022 ambapo Mahakama Sports
wanaume watakutana na timu ya Mipango, huku wanawake wakikabana koo na timu ya
Kilimo kwenye hatua hiyo.
Mshindi kwenye hatua hii atatinga moja kwa moja katika hatua ya
nusu fainali. Akizungumza katika uwanja wa mazoezi, Mwalimu wa Timu Spear
Mbwembe amesema vijana wake wapo kwenye hali nzuri, wanaendelea na mazoezi kama
kawaida na wapo tayari kukabiliana na yoyote atakayepangwa kushindana nao.
“Ninawashukuru sana vijana wangu, wapo vizuri, hatuna majeruhi na
wanatekeleza vyema programu ya mazoezi niliyoiandaa. Ingawa mazoezi ni makali,
lakini wanapokea maelekezo na kwa kweli wanafanya vizuri. Tupo tayari kwa robo
fainali kesho,” amesema.
Mechi zingine zitakazochezwa katika hatua hiyo ya robo fainali kwa
upande wa wanaume ni Uchukuzi watakaomenyana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Kilimo watakutana na TPDC, wakati Ngorongoro watapigishana kwata na Mambo ya
Ndani.
Mshindi kati ya Mahakama na Mipango atakutana na mshindi kati ya
Kilimo na TPDC katika hatua ya nusu fainali, huku mshindi kati ya Uchukuzi na
Tume ya Taifa ya Uchukuzi atakutana na mshindi kati ya Ngorongoro na Mambo ya
Ndani kwenye hatua hiyo.
Kwa upande wa wanawake robo fainali, Tamisemi itakutana na Ocean
Road, TPDC watakabiliana na Ngorongoro, huku Uchukuzi wakijaribu ‘kuchota fedha’
Hazina.
Mshindi kati ya Mahakama na Kilimo atakutana na mshindi kati ya
TPDC na Ngorongoro katika hatua ya nusu fainali ambapo mshindi kati ya Tamisemi
na Ocean road atakutana na mshindi kati ya Uchukuzi na Hazina kwenye hatua
hiyo.
Mahakama Sports imeingia robo fainali baada ya kushinda mechi zake
zote kwenye hatua ya makundi. Mahakama Sports wanaume walimenyana na TPDC na
Tanesco, ambao waliingia mitini kwa kuhofia kipigo, huku Mahakama Sports
wanawake ikiwatambia Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Viongozi ambao wameambatana na Mahakama Sports ni Mwenyekiti Wilson
Dede Makamu Mwenyekiti
Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka,
Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanansolo, Afisa Michezo Nkuruma
Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa na Tiba Teresia Mogani.
Hii inaitwa piga pin syle.
Mahakama Sports wanawake na wanaume (picha ya juu na chini) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazoezi makali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni