Na Faustine Kapama, Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12 Aprili, 2022 amekutana
na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuzungumza nao
mambo mbalimbali, ikiwemo utoaji wa adhabu mbadala na mfumo wa utekelezaji wa mchakato
wa makubaliano (plea bargaining process).
Wakiwa
katika mazungumzo yao, wajumbe hao ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa Tume,
Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe wamemweleza Jaji Mkuu kuwa
kuna sheria nyingi zimetungwa na zingine kufanyiwa marekebisho kuruhusu
Mahakama kutoa adhabu mbadala kwa mtuhumiwa yoyote anapotiwa hatiani kwa kosa
la jinai.
Wamesema
kuwa kutokana na utafiti walioufanya kutoka kwa wadau mbalimbali wamebaini utekelezaji
wa sheria hizo umekuwa hafifu, kwa vile watu wachache ndiyo wanaonufaika na
utaratibu huo. Hivyo wajumbe hao wakaomba kufahamu maoni yake kama Mkuu wa Mhimili
na mambo gani yafanyike kuhakikisha Mahakama inautumia vizuri mfumo huo ili
watu wengi hasa wale waliohukumiwa vifungo ambavyo havizidi miaka mitatu waweze
kunufaika.
Wajumbe
pia waliomba maoni ya Mhe. Prof. Juma kuhusu mfumo wa ‘plea bargaining’ ulivyo,
kama una kasoro na kama kuna kasoro, ipo katika ngazi gani. Jaji Mkuu alianza
kueleza uzoefu wake kuwa katika ziara mbalimbali alizozifanya amegundua Mahakimu
hupata shinikizo kutoka kwenye jamii ambayo inapenda kwamba adhabu kali ndiyo inayopaswa
kutolewa kwa wahalifu.
“Lazima
tuangalie jamii yetu, hata Wabunge wanapenda adhabu kali. Adhabu zetu kwanza ni
kubwa ukilinganisha na Kenya. Utakuta hata zile jitihada za utashi wa kupenda kutoa
adhabu mbadala haziungwi mkono na ukubwa wa adhabu ambazo zinatolewa na Mahakimu
mara nyingi hupata lawama kutoka kwa jamii. Hivyo Mahakimu wanakuwa makini na
jamii inayowazunguka,” alisema.
Amebainisha
vile vile kuwa ukiongea na Wakuu wa Wilaya utagundua wengi kwenye Kamati za Ulinzi
na Usalama hupendelea kuweka watu ndani badala ya kutoa adhabu mbadala. Hivyo Jaji
Mkuu akasema changamoto iliyopo siyo kwa Mahakimu, ambao hujaribu kusoma jamii
inayowazunguka. Mhe. Prof. Juma amesema kuwa pamoja na kutekeleza sheria pia
huangalia utayari wa jamii kupokea wafungwa watakao hukumiwa kutoa huduma
katika jamii.
“Mfano
kama Hakimu akiwaruhusu pengine wafungwa 50 kwenda kutoa huduma za kijamii, je
taasisi za umma zina ule utayari wa kuwapokea na pengine kuwahudumia kwa sababu
wale ni binadamu? Jamii ipo tayari kuwapokea na kuwapa nafasi ya kutoa hizo huduma?
Mimi naona ni msukumo kutoka kwa jamii ambayo uelewa ni mdogo. Kwa hiyo, hili ni
suala la elimu kwa jamii na hata Wabunge wanaotunga hizi sheria,” alisema.
Kuhusu
‘plea bargaining process’, Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa Tume hiyo kuwa mchakato
huo, ambao ni zao la Kamati ya Kanuni ya Jaji Mkuu ni mzuri katika mfumo wa
haki jinai na kwamba tatizo alilopo siyo kwenye sheria yenyewe bali utekelezaji
wa sheria husika. Amesema kitu kilichopotosha suala hilo ni watu kuchukulia dhana
hiyo kama biashara.
“Hii
dhana ya plea bargaining imechukuliwa kama una shilling ngapi, utanipa shilingi
ngapi, badala ya mhusika pengine anakubaliana taarifa za kihalifu, hivyo akiachiwa
kwenye kosa fulani atawapa taarifa ya magenge ya uhalifu, dhana hiyo imejikita
katika kupata fedha. Nadhani wale waliotekeleza mara ya kwanza hawakuelewa
dhana halisi ya plea bargain, ndiyo maana haikushuka kwa watu wa kawaida, ilihusu
fedha kuliko makosa mengine na ilijikita Dar es Salaam zaidi,” alisema.
Kwa
mujibu wa Jaji Mkuu, ukiangalia sheria husika mfumo huo ulitakiwa kusambaa nchi
nzima na siyo mashauri yote kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ambaye hana
uwezo wa kufika huko na kwamba mchakato lazima uwahusishe wale waliofanya
upelelezi, kwa vile wao ndiyo wanaofahamu makosa ambayo upelelezi wake bado
wanaufanyia kazi.
Wajumbe
wengine wa Tume waliohudhuria mazungumzo hayo ni Naibu Katibu-Idara ya Utafiti,
Bw. Kharist Luanda, Naibu Katibu-Idara ya Mapitio, Bw. Lusungu Hongoli na Mtafiti
na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Cleophase Morris.
Naibu Katibu-Idara ya Mapitio kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Bw. Lusungu Hongoli akieleza mfumo wa utekelezaji wa mchakato wa makubaliano (plea bargaining process) mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni