Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Jitihada zinazofanywa
na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma katika kumaliza mlundikano wa mashauri
ndani ya Kanda hiyo zimeanza kuonekana.
Hali hii imejitokeza hivi
karibuni mara baada ya Kikosi kazi ilichoundwa kinachojumusha jumla ya Mahakimu
Wakazi mbalimbali kutoka Kanda hiyo kufanikiwa kumaliza mashauri ya mlundikano 54
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Wilaya Bariadi.
Hatua hiyo inafuatia Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga kuanza kutekeleza mkakati madhubuti
iliyojiwekea wa kumaliza mashauri ya mlundikano (backlog) katika Mahakama zote
ndani ya Kanda hiyo.
Mkakati huo ulifikiwa
mapema mwezi Machi, 2022 katika kikao kazi kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Shinyanga, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wote wa Kanda hiyo.
Baada ya kumaliza kazi
kubwa mkoani Simiyu, leo tarehe 11 Aprili, 2022, kikosi kazi hicho kimehamia katika
Mahakama ya Wilaya ya Maswa, ambapo jumla ya mashauri 10 yameanza kusikilizwa. Miongoni mwa Mahakimu wanaounda kikosi kazi hicho,
Mhe. Christian Lugumira na Mhe Enos Misana, wameanza kusikiliza
mashauri hayo na wanatarajia kumaliza ndani ya siku 14.
Baada ya kumaliza
kusikiliza mashauri hayo ndani ya muda uliopangwa, kikosi kazi cha Mahakimu hao
kitahamia Mahakama ya Wilaya nyingine yenye mashauri ya mlundikano na
kukamilisha ndani ya muda uliokubaliwa katika jitihada za kuondoa mlundikano ndani
ya Kanda ya Shinyanga.
Moja kati ya maazimio
yaliyofikiwa katika kikao kazi ni pamoja na kuanzishwa kwa kikosi kazi maalum
kwa lengo la kumaliza mlundikano wa mashauri yote ya muda mrefu katika Mahakama
zote ndani ya Kanda ya Shinyanga.
Tarehe 14 machi, 2022,
timu ya Mahakimu Wakazi wanne kutoka Mahakama za Wilaya Maswa, Kahama,
Shinyanga na Meatu ilifika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Wilaya
Bariadi kwa ajili ya kuanza kazi ya kuondoa mashauri yote ya mlundikano
yaliyopo katika Mahakama hizo.
Katika hatua nyingine,
ili kukabiliana na ongezeko au uzalishaji mpya wa mashauri ya mlundikano,
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imejiwekea mkakati wa ndani wa kumaliza mashauri
mahakamani ili kukabiliana na suala la mlundikano.
Mahakama za Mwanzo
wamekubaliana kumaliza mashauri ndani ya miezi mitatu toka kufunguliwa hadi
kumalizika. Kadhalika Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya zitamaliza mashauri
mapya ndani ya miezi sita huku Mahakama Kuu ikijiwekea kumaliza mashauri ndani
ya miezi 12.
Kikosi kazi hicho chini
ya uongozi wa Majaji watatu wa Mahakama Kuu kinaendelea na jitihada za kumaliza
mashauri ya mlundikano katika Mahakama zote kwa muda uliopangwa ili kukamilisha
malengo yaliyowekwa ambapo inatarajiwa baada ya muda mfupi Kanda ya Shinyanga
itaandika historia ya kuwa na mashauri ya mlundikano sifuri (0).
Mwonekano wa jengo la
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni