Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Timu ya Mahakama ya
Tanzania, Mahakama Sports) ipo jijini hapa kushiriki katika mashindano ya
michezo mbalimbali ya Mei Mosi kwa mwaka huu wa 2022 yanayofanyika katika Uwanja
wa Jamhuri.
Mweyekiti wa Mahakama
Sports Wilson Dede amesema leo tarehe 18 Aprili 2022 kuwa vijana wake wapo
tayari kwa mashindano hayo ambapo kesho tarehe 19 April, 2022 watajitupa kwa
mara ya kwanza kwenye mchezo wa kuvuta kamba.
Amesema wanawake watachuana
na timu ya Ocean Road, huku Mahakama Sports wanaume wakimenyana na vikali na
timu ya TPDC.
“Vijana wote wapo
tayari kwa mchezo huo. Tumeingia hapa tangu Ijumaa tarehe 15 Aprili 2022 na
kutokana na maandalizi tunayofanya chini ya mwalimu wetu Spia Ngwembe
tunauhakika tutaibuka washindi,” Mwenyekiti huyo alisema.
Amebainisha kuwa jumla
ya timu 15 za kuvuta kamba kutoka taasisi mbalimbali zinashiriki katika
mashindano hayo ambapo timu ya wanaume ya kuvuta kamba ya Mahakama ya Tanzania
imepangwa Kundi B lenye timu tatu.
“Timu za kuvutana kamba
wanaume zipo 15 na kila kundi linatakiwa kuwa na timu nne, hivyo katika kupanga
kwenye vikundi sisi tumeangukia kwenye Kundi B lenye timu tatu linalojumuisha
Timu ya Mahakama, TPDC na Tanesco,” amesema.
Dede amesema kuwa katika
makundi mengine yenye timu nne watacheza mechi tatu lakini kwa upande wa
Mahakama Sports wanaume watacheza mechi mbili.
Kwa upande wa kuvuta kamba
wanawake, Mwenyekiti huyo amesema Mahakama Sports wapo katika kundi A lenye
timu nne zinazojumuisha pia timu za Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na watacheza mechi tatu.
“Baada ya mvutano
kwenye makundi tutaingia kwenye mtoano,” amesema. Ametaja michezo mingine
wanayoshiriki katika mashindano hayo kama bao wanawake, karata wanaume na
wanawake, draft kwa upande wa wanawake na wanaume na pia mbio za wazee.
Jumla ya wachezaji 43 wa
Mahakama Sports wanashiriki katika mashindano hayo. Kati ya hao, wachezaji
wanawake wapo 20 na wanaume wapo 23. Wachezaji wa Timu ya Mahakama wametoka
katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Morogoro,
Shinyanga na Simiyu.
Mwenyekiti Dede
amekumbushia kuwa timu ya kuvuta kamba ya Mahakama ya Tanzania ni mabingwa wa
mashindano ya Shimiwi kwa mwaka 2021.
Amesema miaka ya nyuma
Timu ya Mahakama Sports ilikuwa bingwa, kwa maana kuwa washindi wa kwanza kwa
upande wa wanaume na washindi wa kwanza kwa upande wa wanawake kwa mwaka 2014.
“Tangu kipindi hicho
tulikuwa hatujashiriki katika mashindano haya kutokana na sababu mbalimbali. Tumeamua
kushiriki mwaka huu,” amesema.
Mbali na Mwenyekiti,
viongozi wengine ambao wameambatana na timu hiyo ni Makamu Mwenyekiti Fidelis
Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe
wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanamsolo, Afisa wa timu Nkuruma na Mwalimu
Spia Ngwembe.
Michuano katika michezo
hiyo imechelewa kuanza kutokana na Uwanja wa Jamhuri kuzuiliwa kwa vile ulikuwa
unatumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu. Tayari uongozi wa uwanja umeshatoa
kibali cha kuanzia kutumia uwanja huo
kesho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni