· Yawageuza Ocean Road, TPDC mlenda mchezo wa kuvuta kamba
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 19 April, 2022 imeanza vizuri kwenye mashindano
ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa mara baada ya kuziadhibu
vikali timu za Ocean Road na TPDC katika mchezo wa kuvuta kamba kwa upande wa wanawake
na wanaume.
Ilikuwa timu ya
wanawake iliyoanza kuingia uwanjani majira ya saa moja asubuhi kupambana na
Ocean Road ambapo katika hatua ya kwanza mara baada ya mchezo kuanza Mahakama
Sports ilichukua takribani sekunde tatu tu ndani ya dakika moja kuwanyofoa
wapindani wao kwenye mstari na kuwaacha wakigalagala chini bila kuamini
kilichotokea.
Kazi ilikuwa nyepesi
kwenye hatua ya pili mara baada ya refa kupuliza kipenga kuashiria kuanza kwa
mchezo huo ambapo Mahakama Sports kwa mara nyingine tena ilionekana kuwazindi
nguvu na mbinu za kiushindani wapinzani wao, hivyo kufanikiwa kunyakua pointi
zote mbili.
Baada ya mchezo huo kwa
upande wa wanawake kumalizika, Mahakama Sports wanaume ambayo ndiyo timu pekee
inayoogopwa katika mashindano hayo iliingia kwenye uwanja wa chekecheo na
kufanikiwa kuwachekecha wapinzani wao TPDC ambao hapo awali walionekana
kujiamini kuwa watatoka na ushindi mzito.
Hata hivyo, TPDC
waliangukia pua mara baada ya kibao kugeuka na jahazi lao kuanza kuzama, hivyo kuondolewa
kwenye mstari bila wao kutarajia katika hatua zote mbili, kitendo
kilichowafanya kuanza kulaumiana kwa kushindwa kutekeleza mikakati waliyokuwa
wamepanga na kuachia pointi zote mbili kwa washindani wao.
Akizungumza baada ya
mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema ushindi wa leo kwa
timu zote mbili ni onyo kwa timu zingine pinzani ambazo zimepangwa katika
makundi yao. Timu ya wanawake ipo kundi A huku timu ya wanaume ikiwa imepangwa
kundi B.
“Sisi tunachokiangalia
hapa ni ushindi tu na tupo tayari kupambana na yoyote tutakayekutana naye.
Tumekamilika kila idara na kutokana na maadalizi mazuri chini ya mwalimu wetu
Spear Mbwembe tutatoa kipigo ambacho hakitasahaulika kwa wapinzani wetu. Hata
wao wanajua sisi ni moto wa kuotea mbali,” alisema.
Kwa upande wake,
Mwalimu Mbwembwe aliwataka vijana wake kutokubweteka kwa ushindi huo kwa vile
washindani wao wameonyesha kuwa na nguvu za kiushindani, hivyo wanapaswa
kuchukulia kila mchezo kama fainali.
“Tunamshukuru mungu kwa
kupata ushindi huu, mchezo hasa kwa upande wa wanaume ulikuwa mgumu. Hivyo lazima
tuchukulie kila anayekuja mbele yetu ni fainali, nawomba vijana wangu
wasibweteke, tuendelee kupambana,” alisema.
Katika mechi zijazo
zitakazochezwa, Mahakama Sports wanawake watapambana na Tanesco kesho tarahe 20
Aprili, 2022 na baadaye tarehe 22 Aprili, 2022 kukutana na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, huku timu ya wanaume ikikutana uso kwa uso na timu ya Tanesco siku
hiyo ya tarehe 22 Aprili, 2022.
Katika mashindano hayo
kwa upande wa wanawake, timu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliibuka na ushindi
dhidi ya Tanesco, Afya nayo ikaigalagaza Hazina huku Uchukuzi ikiibuka kidedea
dhidi ya Sanaa, Tamisemi wakashinda dhidi ya Ngorongoro na TPDC wakapata
ushindi wa bure mara baada ya Tarura kuingia mitini na Kilimo kupata ushindi
dhidi ya Maji.
Kwa upande wa wanaume,
Ngorongoro waliibuka na ushindi dhidi ya wenzao Maliasili, Mipango wakaishinda Maji,
huku Kilimo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakipata ushindi wa bure dhidi ya
Tarura na Ukaguzi, mtawaliwa, ambao hawakutokewa uwanjani, Uchukuzi wao
wakaibuka na ushindi dhidi ya Utamaduni huku Hazina wakiangukia pua dhidi ya Mambo
ya Ndani iliyopata ushindi.
Mbali na Mwenyekiti,
viongozi wengine ambao wameambatana na timu hiyo ni Makamu Mwenyekiti Fidelis
Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe
wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanamsolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja
wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa Teresia Mogani.
Mahakama Sports wanaume wakichuana vikali na wapinzani wao TPDC (hawapo katika picha) leo tarehe 19 Aprili, 2022 kwenye mchezo wa kuvuta kamba katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mahakama Sports imejizolea pointi zote mbili mara baada ya kuwashinda wapinzani wao katika hatua zote mbili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni