Jumatano, 20 Aprili 2022

MAHAKAMA SPORTS WANAWAKE WAIFUMUA TANESCO

 Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) ya wanawake leo tarehe 20 April, 2022 imeendelea kutoa dozi kwenye mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa mara baada ya kuiwapulizia pumzi ya moto timu ya Tanesco katika mchezo wa kuvuta kamba.

Mchezo huo ulianza majira ya saa 12.30 asubuhi kuzikutanisha timu hizo ambapo katika hatua ya kwanza Mahakama Sports chini ya Mama Mchawi Mwanansolo haikuwachukua hata sekunde mbili kuwanyofoa wapinzani wao kwenye mstari mweupe.

Kadhalika katika hatua ya pili, Tanesco haikuonesha upinzani wowote, hivyo wakalazimika ‘kuzitapika’ pointi zote mbili kwa wapinzani wao, ambao tangu awali walionesha kujiamini na kucheza mchezo huo kama timu.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema, “Mimi huwa sipendi kusema mengi, nadhani hata wewe umeona jinsi vijana wetu walivyokuwa na ari ya mchezo. Hatuna kingine zaidi ya kutoa dozi. Tunawaomba wapinzani wetu watulie ili sindano iwaingie vizuri.”

Mwenyekiti Dede amewaomba vijana wake kuendelea kuzingatia programu ya michezo iliyoandaliwa na mwalimu Spear Mbwembe na kuhakikisha kila mpinzani atakayejitokeza kupambana nao anapata dozi yake anayostahili.

Mmoja wa Waamuzi wa mchezo huo amewasifia Mahakama Sports Wanawake kwa kujituma na kucheza kitimu. “Hawa watafika mbali sana. Wapo vizuri, wanajituma, nahisi wana mwalimu mzuri. Waone!!! wote wana nguvu na stamina kwenye miguu, wakishika kamba huwezi kuwang’oa kirahisi,” alisikika akisema.

Mahakama Sports wanawake imebakiza mchezo mmoja ambao utachezwa tarehe 22 Aprili, 2022 na kukutana uso kwa uso na timu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Siku hiyo hiyo, Mahakama Sports wanaume watakabiliana na timu ya Tanesco.

Katika mechi zingine zilizochezwa leo kwa upande wa wanawake, Uchukuzi wameibuka washindi dhidi ya Afya, huku Ocean Road wakiibuka wababe kwa timu ya Taifa ya Uchaguzi, Hazina wao wamewashinda Utamaduni, Tamisemi wakaambulia pointi moja baada ya kutunishiana misuri na Tanroads katika hatua ya pili.

Michezo mingine iliwajumuisha NCAA walioibuka washindi dhidi ya Mambo ya Ndani, huku TPDC wakishinda dhidi ya Waziri Mkuu, Mipango nao wakashinda dhidi ya Utamaduni na Kilimo wakapata ushindi wa mezani mara baada ya Tarura kuingia mitini, ambapo Maji waliibuka kidedea dhidi ya Waziri Mkuu.

Kwa upande wa wanaume, Uchukuzi waliifurusha Mipango, TPDC wakaishinda Tanesco, Kilimo wakaibwaga Ukaguzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakaibuka wababe wa Tarura, huku Utamaduni wakaambulia kichapo kutoka kwa Hazina.

Wengine walikuwa NCAA wakashinda dhidi ya Maji, Utamaduni wakaangukia pua kwa Hazina, Maliasili wakagalagazwa na Mipango na Uchukuzi wakaibuka wababe wa Mambo ya Ndani. Leo Mahakama Sports wanaume hawakucheza.

Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana na timu hiyo ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanansolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa Teresia Mogani.


Mmoja wa Waamuzi akiziamuru timu za Mahakama Sports wanawake na Tanesco kushika kamba wakati wa mpambano wao leo tarehe 20 Aprili, 2022. Timu ya Mahakama iliibuka mshindi na kujinyakulia pointi zote mbili.
Mahakama Sports wanawake wakiwakamua Tanesco.
Timu ya Tanesco wakipokea pumzi ya moto kutoka timu ya Mahakama Sports wanawake.
Mahakama Sports wanawake wakiserebuka mara baada ya kuwazabua Tanesco.
Ukisikia raha ya ushindi ndiyo hii sasa.

Mahakama Sports wanawake chini ya Mama Mchawi Mwanansolo (wa kwanza kushoto waliosimama)wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mchezo na Tanesco.

Mahakama Sports wanawake na wanaume wakiwa jukwaani wakiangalia timu zingine zinavyoteseka!!

Timu ya Afya wakiwa chini baada ya kugalagazwa na Uchukuzi.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni