Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka leo tarehe 21 Aprili, 2022 amezindua rasmi
mashindano
ya michezo mbalimbali ya Mei Mosi kwa mwaka huu wa 2022 yanayofanyika katika
Uwanja wa Jamhuri jijini hapa na kuhimiza wanamichezo
wote kushiriki kikamilifu, kwani michezo ni ajira, furaha na afya.
Akizungumzia
katika uzinduzi huo, Mhe. Mtaka amewashuruku viongozi waliondaa mashindanio
hayo, akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi, Mhe, Dkt. Hamis
Mkanachi kwa kuweka Kauli Mbiu ambayo inahamasisha wananchi kushiriki katika
shughuli mbalimbali, ikiwemo michezo, sensa na chanjo dhidi ya ugonjwa wa
korona.
Amenukuu
Kauli Mbiu hiyo inayosema, “Michezo ni Afya na Huamsha Ari ya Kazi, Cheza,
Chanja na Hesabiwa,” na kusema kuwa yeye huwa hakubaliani na mambo ya michezi
ni afya na ndiyo maana wachezaji waliopo huwa hawafanyi vizuri katika michezo
mbalimbali, ikiwemo ya Ligi Kuu.
“Tunaenda
UMISHUMITA kesho kutwa, mtu yupo Darasa la Nne na anakipaji cha kucheza, lakini
anaambiwa michezo ni afya, michezo ni furaha. Hizi furaha kila mmoja anazo kwa
namna yake. Tukianza kuwajenga wajue kwamba michezo ni biashara, michezo ni
ajira, inaweza ikawa jambo la maana zaidi,” amesema.
Kwa
mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, haishangazi kuona sehemu kubwa ya wachezaji kwenye
Ligi wanaofanya vizuri bado ushindani wa
wale wanaotoka nje na waliopo ndani ni mkubwa, maana mchezaji hukaa pale
uwanjani akicheza kiafya, afya, au kifuraha, furaha.
“Kwa
hiyo, kwangu mimi (nashauri) tuanze kubeba kauli mbiu ya michezo ni ajira,
michezo ni burudani ili kama hapa kuna mzazi ana mtoto anacheza ajue kwamba
atapata A ya kucheza vizuri kama anavyopata A ya darasani,”amesema.
Mhe.
Mtaka amesema uzinduzi huo ni mwanzo rasmi katika safari kuelekea kilele cha
siku ya Mei Mosi na kwamba kuna matukio mengi ambayo yamepangwa kama Mkoa
kuelekea siku hiyo.
“Moja
ni shughuli hizi za kimichezo na pili kesho tutaanza maonyesho ya shughuli na
bidhaa mbalimbali kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete Convention ambapo kuna
waonyeshaji zaidi ya 300 watakaokuwa pale kwa ajili ya kusherehesha kuelekea
Mei Mosi,” amesema.
Hivyo
amewashukuru wakuu wote wa taasisi, viongozi wa serikali na sekta binafsi kwa
kuridhia watumishi wao kuja Dodoma kushiriki katika shughuli za kimichezo kulelekea kilele cha Mei Mosi.
Mhe.
Mtaka ametumia fursa hiyo kukumbushia kuwa alipokuwa akizindua siku rasmi
itakayofanyika sensa ya watu na makazi,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
aliwaelekeza viongozi wote wa serikali
na wadau wote kutumia kila aina ya mikosanyiko ya watu kuwahabarisha
Watanzania kuhusu sensa, hivyo amewaomba wananchi wote kujiandaa kuhesabiwa.
Kuhusu
chanjo, Mkuu wa Mkoa amewaambia wanamichezo waliofurika katika Uwanja wa
Jamhuri kuwa uhai wa binadamu sio mali ya serikali, kanisa wala msikiti na
kuwakumbusha ipo siku watakufa na kuuacha msikiti, kanisa na serikali, hivyo suala
la kuchanja ni kwa faida ya mtu mwenyewe kwa kujua anabeba dhamana ya familia
na maisha yake.
“Hivyo
tukumbushane kuchanja ni kwa faida yako, kama utaweza kucheza na afya yako ni
wewe mwenyewe na mapungufu yako. Mtu aliyechanja huwa amejizuia na hatari kubwa
zaidi tunapokuwa kwenye mikusanyiko mikubwa kama hii,”amesema.
Aliongelea
pia suala la sensa ambapo kwa sasa zoezi linaloendelea ni kutambua mali za watu
na makazi, hivyo akatumia hadhara hiyo kuhimiza kila mmoja kutoa ushirikiano
katika zoezi hilo.
“Tutoe
ushirikiano wa dhati kwa viongozi wa serikali wanaokuja kwenye maneo yetu kwa
ajili ya kutambua barabara, mitaa na nyumba ili kuweka utambuzi na utambulisho
wa makazi na watu wajitokeze siku ya sensa na kutoa ushirikiano unaostahili,”
Mhe. Mtaka alisema.
Akiwa
katika uwanja huo, Mkuu wa Mkoa huyo alicheza penati kuashiria uzinduzi rasmi wa
michezo hiyo na kufanikiwa kumtungua kipa wa timu ya Ngorongoro aliyekuwa
ameandaliwa kwa ajili ya tukio hilo.
Kabla ya sherehe hizo za uzinduzi, wanamichezo wote walishiriki katika maandamano yaliyoanzia viwanja vya Nyerere Square na kuishia katika Uwanja wa Jamhuri.
Uzinduzi
huo umehudhuriwa na viongozi kutoka sekta na taasisi mbalimbali za serikali na
Mahakama, akimwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma,
Mhe. Gerson Mdemu, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda, Mhe. Silvia Rushasi na Mwenyekiti wa
Michezo wa Mahakama, Mkoa wa Dodoma, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe.Denis
Mpelembwa.
Viongozi
wa Mahakama Sports walioongoza wanamichezo wa Mahakama ya Tanzania kwenye
uzinduzi huo ni Mweyekiti
wa Mahakama Sports Wilson Dede, Makamu
Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia
Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanansolo, Afisa Michezo
Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume, Meneja Vifaa Teresia Mogani na
Mwalimu Spear Mbwembwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni