· Tanesco wakata umeme, waingia mitini
· Mahakama wanawake waipigisha kura NEC
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Timu
ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 22 April, 2022 imeendeleza
ubabe katika mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini
hapa mara baada ya kuzoa pointi zote muhimu kwenye mchezo wa kuvuta kamba
wanaume na wanawake.
Tanesco
waliokuwa wamepangwa kupimana umwamba na Mahakama Sports wanaume walilazimika kukata
umeme na kuingia mitini, huku Mahakama Sports wanawake wakaisambaratisha Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hivyo kila timu pinzani kuachia pointi zote mbili
kwa wababe hao kutoka Mhimili wa kutoa haki nchini.
Mechi
ya kwanza iliwakutanisha Mahakama Sports wanawake majira ya saa moja asubuhi
ambapo katika hatua ya kwanza NEC walijaribu kujitutumua lakini wakakumbana na
kipigo kikali kilichowafanya washindwe kuelewana, hivyo kupururwa kirahisi na
kutoka kwenye mstari mweupe.
Katika
hatua ya pili, NEC walionekana kuchanganyikiwa kutokana na kushindwa kila mbinu
waliyojaribu kuitumia ili kuwatoa Mahakama Sports kwenye mchezo na kuwaacha
wababe hao wakiondoka na pointi zote mbili muhimu katika mashindano hayo.
Baada
ya timu za wanawake kumalizika, Waamuzi walianza kuita wanaume, huku timu ya
Mahakama Sports ikipangwa ya tatu na Tanesco. Mchezo huo ulipowadia, Mahakama
Sports walionekana pekee yao kwenye ulingo na kusababisha Waamuzi hao
kuuahirisha kwa muda ili kuwapa nafasi Tanesco kujipanga.
Mchezo
huo ulipangwa wa mwisho katika hatua hiyo, lakini licha ya kuitwa mara kadhaa kupimana
ubavu na miamba hiyo ya Mahakama, Tanesco walitoweka ghafla katika mazingira ya
kutatanisha na kujibanza kusikojulikana, hivyo kuruhusu Mahakama Sports kupewa
ushindi wa mezani.
Akizungumza
baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede alisema,
“Tanesco hawajatutendea haki hata kidogo. Sisi ni wapenda haki daima na kazi
yetu ni kutoa haki. Tulitaka tukutane nao hapa ili sio tu haki itendeke, bali pia
ionekane imetendeka. Wanabahati sana hawa.”
Tangu
yalipoanza mashindano hayo, Mahakama Sports wanawake wameshakuta na timu za
Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, huku Mahakama Sports wanaume
wakimenyana na TPDC na Tanesco. Katika mechi zote hizo, Mahakama Sports
wameibuka washindi.
Kufuatia
kumalizika kwa hatua hii ya makundi, mashindano sasa yanaingia katika hatua ya
mtoano wa timu 16 bora. Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu
itakayopoteza katika hatua hii itakuwa imeyaaga mashindano kwa ujumla. Mechi za
mtoano zinatarajiwa kuanza tarehe 25 Aprili, 2022 ili kupisha michezo mingine
itakayoanza kesho kama riadha, bao, karata na minigine.
Michezo
mingine ya kamba iliyochezwa leo kwa upande wa wanawake ilikuwa Ocean road
walioshinda dhidi ya Tanesco, Hazina walioshinda dhidi ya Mipango, Utamaduni
wakaangukia pua kwa Afya, Ngorongoro wakiibuka wababe wa Tanroads, Mambo ya
Ndani wakishindwa kufurukuta kwa TAMISEMI na TPDC wakiwashinda Kilimo.
Kwa
upande wa wanaume, Tume ya Taifa ya Uchaguzi waliwabamiza Tume ya Utumishi
Walimu, Maliasili ikashinda dhidi ya Maji, Mgorongoro wakaibuka wababe wa
Mipango, Uchukuzi wakashinda dhidi ya Hazina, Mambo ya Ndani wakawapigisha
kwata Utamaduni na Kilimo wakawalimisha Tume ya Utumishi ya Walimu.
Mbali
na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana na Mahakama Sports ni Makamu
Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia
Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanansolo, Afisa Michezo
Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa Teresia Mogani.
Mahakama Sports wanaume wakiwa tayari kuwakabiri Tanesco kwenye kichekecheo. Tanesco waliingia mitini baada ya kuhofia kichapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni