Na Innocent Kansha - Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani amewataka wamiliki wa malengo ya kimkakati wote ndani ya
Mahakama kutekeleza Mpango Mkakati wa awamu ya pili wa mwaka 2020/2021 hadi
2024/25 zilizopo chini yao kikamilifu ili zikamilike kwa muda uliopangwa.
Akiwasilisha taarifa fupi ya mafanikio ya Mpango
Mkakati wa awamu ya kwanza wa mwka 2015/16 hadi 2020/2021 kwa wajumbe wa kikao
kazi cha mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa
uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 jana tarehe 4
Aprili 2022 Jijini Arusha, Jaji Siyani alisema, kwa kuwa wao ndiyo wataalamu
katika maeneo yao, Mahakama inatarajia watafanya tafiti za kina na hivyo kuibua
mikakati mizuri ya utekelezaji wa kazi zao kwa weledi mkubwa.
“Kwa kuwa sote tunajenga nyumba moja na nia yetu ni
moja niwaase wenzetu wa Kitengo cha Maboresho (JDU) na wamiliki wa malengo ya
kimkakati (SO-Owners) kuimarisha mahusiano baina yao” alisema Jaji Kiongozi
Mhe. Siyani akaongeza kuwa ni vema JDU na wamiliki
wa malengo ya kimkakati wawe na mtazamo chanya katika utekelezaji wa majukumu
yao ili wanakutana na changamoto zozote zitakazojitokeza waweke meza ya pamoja
na kuzitafutia ufumbuzi.
Jaji Siyani akafafanua kuwa, ili Mahakama ifanikiwe
katika utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa uboreshaji lazima kazi zote
zinazotekelezwa zijulikane kwa Viongozi na watumishi wa Mahakama wa ngazi zote
na wajibu na majukumu ya kila mmoja yakabainishwa wakati huu wa kuweka mipango
ya utekelezaji.
Amesema SO Owners wote watapaswa kumiliki ipasavyo
shughuli zao na kuzitekeleza kwa ufanisi mkubwa na kasi iliyokusudiwa hasa
wakizingatia kwamba muda wa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa Mahakama
awamu ya pili ni mfupi sana takribani miaka mitatu (3) na una fedha nyingi
ukilinganisha na miaka mitano ya awamu ya kwanza.
Aidha, Jaji kiongozi akawakumbusha watekelezaji wa
Mpango Mkakati kuwa ucheleweshaji wa shughuli za mradi wa uboreshaji zinatokana
na watekelezaji kutomiliki ipasavyo shughuli za wanazotakiwa kuzitekekeleza na
kuzikasimu kwa Maafisa wa chini.
"Mfano maandiko mengi (Concept notes)
zilizowasilishwa JDU bila wamiliki wa malengo ya kimkakati kuzipitia vizuri
ilipelekea maandiko hayo kurejeshwa tena kwao kwa ajili ya kurekebishwa na
kusababisha kuchelewesha utekelezaji wa shughuli husika," alisema.
Mhe. Siyani akawaasa watekelezaji wa mradi kutatua
changamoto ya umiliki mdogo wa shughuli za mradi (low ownership)
zinazotekelezwa kwenye maeneo mbalimbali.
Alisema hilo lilidhihilishwa na Viongozi mbalimbali
wa Mahakama kutokuwa na taarifa za kina za miradi inayatekelezwa na katika
maeneo husika na hivyo kushidwa kusimamia ipasavyo miradi hiyo.
"Kwa kiasi kikubwa jambo hili lilichangiwa na
ushirikishwaji hafifu na pia Viongozi wa Kanda kuona kuwa masuala ya maboresho
ni ya Makao Makuu na wao hayawahusu," Jaji Kiongozi huyo amesema.
Kwa mujibu wa Jaji Siyani, kwa kuwa utekelezaji wa Mpango Mkakati sio suala la Makao Makuu pekee bali ni la Mahakama zima hivyo baadhi ya kazi zitashushwa chini (Cascading) ili zitekelezwe na kila mmoja wenu kwa ufanisi mkubwa.
Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Mpango Mkakati pamoja na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama utategemea zaidi kujitoa kwa kila Kiongozi, Mtumishi na Wadau wa Mahakama na kuongeza ushirikiano katika ngazi zote.
Jaji Kiongozi akawakumbusha wote wanahusika na uboreshaji kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa kutosha baina yao, Viongozi wote wa Mahakama kwa ngazi mbalimbali wahakikishe wanajihusisha na usimamizi wa shughuli zote zinazotekelezwa katika maeneo yao, kama ambavyo zitakuwepo kazi zitakazo gatuliwa kwao ili zitekelezwe.
"Bila kuacha shaka kazi hizi zitaenda sambamba na kufanya ukaguzi, kutoa ushauri na mapendekezo ya namna bora zaidi ya kufanikisha utekelezaji wa miradi husika katika maeneo mbalimbali inakotekelezwa na kutoa taarifa za miradi hiyo kwa wakati ili maamuzi sahihi yaweze kufanyika kwa wakati," alisisitiza Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akifungua kikao kazi cha siku ya pili cha wajumbe wa mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili na Mradi wa uboreshaji huduma za Mahakama awamu ya pili 2022/2023 – 2024/25 jana tarehe 4 Aprili 2022 Jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni