Jumamosi, 14 Mei 2022

ANDAENI BAJETI SHIRIKISHI: JAJI MLACHA

Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha amewataka wajumbe wa kikao cha Kamati ya bajeti ya Kanda hiyo kuandaa mipango na bajeti ambayo ni shirikishi iwe rahisi kutekelezeka.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Kanda hiyo tarehe 13 Mei, 2022 katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Mlacha aliwasihi wajumbe kuwa wabunifu na kuzingatia eneo la motisha kwa watumishi ili kuongeza ari na nguvu ya kufanya kazi.

Aliongeza kuwa, wajumbe hao wanalo pia jukumu la kuandaa mpango kazi wa mwaka 2022/2023 (Action plan) na mpango wa manunuzi ili kurahisisha utekelezaji wa bajeti kwa ajili ya kuandaa Mipango na Bajeti ya utekelezaji wa majukumu ya Mahakama Kanda ya Kigoma kwa mwaka 2022/2023.

“Andaeni mpango kazi (Action plan) ili kusaidia kujua kazi gani itafanyika lini na kwa rasilimali zipi chini ya usimamizi wa nani” alisema Jaji Mlacha

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwafahamisha wajumbe hao kwamba, Mahakama za Wilaya ya Buhigwe, Kakonko na Uvinza zinatarajiwa kufunguliwa mwaka wa fedha 2022/2023 hivyo wanatakiwa kuandaa bajeti ya Mahakama hizo pia. Hali kadhalika alihimiza bajeti inayoandaliwa ilenge kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Jaji Kiongozi kuhusu kurejesha huduma za Mahakama kwenye Mahakama za mwanzo zilizofungwa angalau Mahakama mbili kwa kila Wilaya.

Kwa upande mwingine, Jaji Mlacha aliwaasa wajumbe wa kikao hicho kuweka gharama halisi kulingana na mabadiliko ya hali ya maisha ili kuepuka baadhi ya vifungu kuishiwa fedha mapema.

Naye mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo alisema kuwa maandalizi ya bajeti hizo yatazingatia miongozo yote iliyotolewa ya uandaaji wa bajeti na kuweka vipaumbele kulingana na mipango ya Mahakama ya Tanzania na ile ya Kanda ambapo pamoja na maeneo mengine eneo la  uondoshaji wa mashauri mlundikano, masuala ya TEHAMA na stahili kwa watumishi yakiwa kipaumbele.

Kamati za bajeti zimeanzishwa ili kuleta chachu ya kuhakikisha kunakuwepo  mipango na bajeti yenye kuakisi hali halisi ya mahitaji ya utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kuweka uwazi na ushirikishwaji wa watumishi katika kupanga na kutekeleza bajeti hivyo kuwa na udhibiti  wa pamoja wa rasilimali fedha zilizotengwa katika maeneo husika.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe.  Lameck Mlacha(Katikati) akifafanua jambo wakati alipokuwa akifungua kikao cha ya bajeti Kanda ya Kigoma. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama-Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka na Kushoto ni Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Gadiel Mariki.

 Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kibondo, Bi. Naomi Chawe  akitoa ufafanuzi wa bajeti ya Mahakama ya Wilaya hiyo na Mahakama tarajiwa ya Kakonko katika kikao hicho.

Wajumbe wa kikao wakimsikiliza Mhe. Jaji Mfawidhi (hayupo katika picha) wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati ya bajeti.
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni