·Yanyakua medali baada ya kushika nafasi ya pili
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) jana terehe 14 Mei,
2022 iliacha gumzo kwenye Bonanza lililoandaliwa na Chama cha Mawakili
Tanganyika (TLS) mara baada ya kuibuka washindi wa pili kwenye mchezo wa mpira
wa miguu (Soka).
Bonanza hilo lilioshirikisha timu mbalimbali ikiwemo ya Mahakama
Sports, Chuo kikuu cha Dar es salaam, TLS na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lilifanyika
katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (Mlimani). Katika mchezo huo wa
soka, timu shiriki zilicheza kwa mtoano ambapo timu iliyoshinda katika hatua
hiyo itiingia moja kwa moja fainali.
Katika hatua ya mtoano, TLS ilipangwa kucheza na timu ya Mamlaka
ya Mapato Tanzania, huku Mahakama Sports ikamenyana na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Ilikuwa timu ya TLS iliyofanikiwa kutinga fainali mara baada ya
kuwabanjua TRA kwa goli moja kwa sifuri.
Kwenye mchezo uliozikutanisha Mahakama Sports na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, timu ya Mahakama Sports walishinda kwa goli mbili kwa moja, hivyo
kufanikiwa kutinga katika hatua ya fainali. Magoli ya Mahakama Sports yalifungwa
na mshambuliaji hatari Robert Tende.
Kufuatia matokeo hayo, Mahakama Sports ilikutana na TLS katika
hatua ya fainali ambapo ndani ya dakika 90 timu zote zilitoka kwa kufungana
goli moja kwa moja na goli la Mahakama Sports likifungwa kwa mara nyingine na
Robert Tende aliyeonekana kuwa mwiba kwa timu pinzani.
Baada ya kutoka sare ndani ya dakika hizo 90, Mwamuzi aliamuru
kupigwa mikwaju ya matuta (penalty), ambapo
Mahakama Sports walipata magoli mawili huku TLS wakabahatisha magoli matatu,
hivyo TLS kutangazwa kuwa mabingwa wa Bonanza hilo.
Wachezaji walioshiriki kwenye mchezo huo walikuwa Spear Mbwembwe, Florence Gisbert, Mohamed Migomba, Jamal Mkumba, Said Albea, Ghulam Katwila, Omari Mdakama, Rajabu Ally, maarufu kama Roja Kumbakumba, Fidelis Choka, Robert Tende na Antony Mfaume. Wachezaji wa akiba walikuwa Wilson Dede, Magesa Mgeta, Ferdinand Philip, Mohamed Burhan, Goodluck Mushi na Victor Zacharia Mchopa.
Akiongea baada ya mechi hiyo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson
Dede amewapongeza wachezaji wote kwa kujituma na kufanya vizuri kwenye Bonanza
hilo licha ya kupata mwaliko kwa muda mchache na kufanya mazoezi kwa muda mfupi.
“Niwapongeze vijana wangu kwa kufanya vizuri kwenye Bonanza hili
ingawa tulipata mwaliko kwa muda mfupi. Hii ni salamu tosha kwa timu pinzani
kwamba Mahakama Sports tupo vizuri. Tunatanguliza pia salamu zetu kwa wapinzani
wetu kwenye mashindano yajayo ya SHIMIWI. Safari hii tunaenda kuwashangaza,
hawataamini kitakachowakuta,” alisema.
Mbali na mwenyekiti huyo, viongozi wengine walioambatana na timu
ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Mhasibu Rajabu
Dihwa, Meneja wa Timu Anthony Mfauke na Mtunza Vifaa Thedy Morgan.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni