Na Magreth Kinabo- Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani amewataka watumishi wote wa mahakama nchini, kuendelea kuwatumikia
Watanzania kwa juhudi na maarifa yanayoendana na mazingira ya karne ya 21.
Hayo yamesemwa na Jaji Kiongozi wakati akizungumza kwenye
mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masijala Kuu, ambao ni wa mara
ya kwanza kufanyika, uliofanyika
mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Morogoro, ambapo alisema karne hiyo ni ya ushindani
katika utoaji wa huduma bora.
‘‘Ni lazima wafanyakazi tujibadilishe sio tu kifikra
bali tufanye kazi katika namna ambayo itawezesha wale wale tunaowahudumia
kuridhika. Ni kwa kufanya hivyo tu, tutakuwa na haki ya kuendelea kuwahudumia. Sasa
kwa wafanyakazi wa mahakama, sera na mwelekeo wetu ni kuimarisha matumizi ya
teknolojia katika utoaji haki,’’ alisema Jaji Kiongozi.
Aidha Jaji Kiongozi alisema mafunzo mbalimbali
yametolewa na yataendelea kutolewa katika eneo hilo, hivyo kila mtumishi bila kujali
kada yake, atambue, kuwa anao wajibu wa kuhakikisha azma hiyo inatimia.
Alifafanua kwamba kila mtumishi anapaswa kujua kuwa
lengo letu ni kuhakikisha kuwa watu wote wanaokuja kubisha hodi katika milango
ya mahakama, wanapata haki kwa wakati na yoyote atakayekuwa kikwazo katika
kufikia lengo hilo, hafai kuwa mtumishi wa karne ya 21.
Jaji Kiongozi huyo aliongeza kazi ya msingi ya Mahakama
ni kutoa haki kwa kupokea na kusikiliza mashauri mbalimbali.Mahakama
inafanyakazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kutimiza jukumu hilo,
Mahakama ina Mpango Mkakati ambao ni budi kila mmoja wetu kuujua na mradi wa
maboresho unaoendelea.
‘‘Kwa kuwa watumishi ndio watekelezaji wa yote
yanayoamuliwa na uongozi ikiwemo mradi wa maboresho, ni rai yangu kwamba
mabaraza kama haya sio tu yajadili maslahi ya wafanyakazi, lakini yatumike pia
kama sehemu ya kukumbushana mipango mbalimbali na mambo ya msingi kazini ili
mfanyakazi awe sehemu ya mafanikio ya taasisi,’’ alisitiza.
Kwa upande wake Katibu wa TUGHE wa Mahakama ya
Tanzania, Bw. Michael Masubo akiwakilisha hoja za wafanyakazi wa mahakama hiyo
kwenye baraza hilo, alisema semina za watumishi zitolewe mara kwa mara ili
kuwajengea uwezo katika kazi zao za kila siku, mishahara kuwa katika ngazi moja,utoaji
wa elimu kuhusu maboresho ya Mahakama yanayoendelea kwa watumishi ili waweze kuijua Mahakama yao, na
suala la upandishaji vyeo.
Mahakama ya Tanzania umetekeleza Mpango Mkakati wa
Miaka Mitano 2015/16 – 2019/20 na Maboresho ya Mahakama wa 2016/17-2021/22. Hivi
sasa imeanza utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango Mkakati wa 2020/21- 2022/25
na Mradi wa Maboresho ya Mahakama wa Awamu ya pili wa 2022/23- 2024/25.
Baadhi ya watumishi wa mahakama hiyo wakiwa katika mkutano huo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Mustapher
Siyani, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya majaji na
watumishi wa mahakama hiyo mara baada ya kufungua mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni