Na. Faustine Kapama, Mahakama, Tanga.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 16 Mei, 2022 ameanza
ziara ya kikazi ya siku nne katika Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Tanga,
kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja na
kuongea na watumishi na wadau mbalimbali.
Kakika
siku yake ya kwanza, Mhe. Jaji Mkuu amemtembelea Mkuu wa Mkoa, Mhe Adam Malima na
kufanya naye mazungumzo mafupi kabla ya kuelekea Pangani kukutana na Mkuu wa
Wilaya hiyo, Mhe. Ghaibu Lingo. Baada ya hapo, Jaji Mkuu aliekelekea katika Mahakama
ya Wilaya ya Pangani ambapo alipokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joel Mguto.
Akiwa
katika Mahakama hiyo, Mhe. Prof. Juma alipata fursa ya kuongea na watumishi
kabla ya kuelekea Wilaya ya Muheza ambapo alikutana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe.
Halima Bulembo na baadaye kuongea na watumishi katika Mahakama ya Mwanzo na
Mahakama ya Wilaya ya Muheza.
Kabla
ya kuongea na watumishi wa Mahakama hizo, Jaji Mkuu alipokea taarifa ya
utendaji kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Mhe. Lilian
Rutehangwa ambaye ameainisha mafanikio waliyofikia ikiwemo kusikiliza mashauri
kwa wakati, kuendesha shughuli za kimahakama kupitia fedha za matumizi ya
ofisi, kutoa nakala za hukumu kwa wakati kwa wadaawa na upatikanaji wa vitendea
kazi, mfano komputa.
Ameelezea
mikakati waliyonayo inayojumuisha kutokuwa na mludikano wa mashauri, kuboresha
majengo kwa kufanya ukarabati mdogo kadri wanavyopokea fedha za matumizi,
kulipa stahiki mbalimbali za watumishi na upatikanaji wa vitendea kazi kwa
wakati na vya kutosha kwa Mahakama zote.
Akiongea
na viongozi wa Serikali kwa nyakati tofauti, Mhe. Prof. Juma alisisitiza
umuhimu wa wadau katika mnyororo wa utoaji haki kusoma hukumu mbalimbali
zinazopatikana bure katika mtandao wa Mahakama ambazo zimesheheni masuala muhimu
yanayosaidia kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi, husuani katika mashauri ya
mirathi na dawa za kulevya.
Amewaeleza
viongozi hao kuwa Kikao cha Mahakama ya Rufani kilichoketi Tanga hivi karibuni
kimebaini mashauri yanayohusu dawa za kulevya ndiyo yanayoongoza katika Kanda
hiyo ya Mahakama, hivyo akashauri vyombo vinavyohusika na upelelezi kufuata
sheria na taratibu katika kushughulikia kesi hizo ili kuwezesha haki kutendeka zinapofikishwa
mahakamani.
“Mkoa
huu unachangamoto ya kesi za dawa za kulevya na changamoto kubwa tunazoziona ni
namna gani ushahidi unavyokusanywa. Wakati mwingine kuna makosa ambayo yanayojirudiarudia
katika ukusanyaji wa ushahidi, ambayo yanasababisha wakati mwingine wale
wanaohusika kuachiwa huru. Hii wakati mwingine inafanya wananchi wasielewe. Hivyo,
viongozi wasome zile hukumu ili waone maeneo ya changamoto hizo ambazo
zimeonyeshwa,” alisema.
Akiwa
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Prof. Juma alipata taarifa za msiba wa mmoja
wa madiwani katika halimashauri ya Manispaa ya Tanga, ambaye ni ndugu wa karibu
na Jaji Mkuu mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman. Kutokana na taarifa hiyo,
Jaji Mkuu aliamua kukatisha ziara yake kwa muda na kwenda kutoa pole kwa
familia na wanaombolezaji waliokuwa kwenye msiba huo.
Katika
ziara hiyo, Jaji Mkuu anatarajia pia kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya
za Kilindi, Handeni, Lushoto na Korogwe kabla ya kuhitimisha ziara yake Tanga
mjini. Mhe. Prof. Juma ameongozana na viongozi
mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Kevin Mhina, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama,
Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama
ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba.
Wengine
ni Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi
Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory
Kagaruki, mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury,
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Bw. Yohana Mashausi, Afisa Utumishi, Bw. Jeofrey
Mnemba, Mpima Ramani Abdallah Nalicho, Mhandisi Peter Mrosso na Msaidizi wa
Sheria wa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Hassan Chuka.
Kwa
upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa
Mansoor, Naibu Msajili Beda Nyaki, Mtendaji Humphrey Paya, Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Sofia Masati na Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Mhe. Ruth Mkusi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni