Na. Faustine Kapama– Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda jana tarehe 27 Mei,
2022 ameongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama hiyo kupokea na kujadili
taarifa za utendaji zilizowasilishwa na viongozi mbalimbali.
Katika kikao hicho, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania kwenye Divisheni hiyo, Bi. Masalu Kisasila aliwapitisha wajumbe wa Baraza
hilo kwenye mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021/2022-2024/2025) wa Mahakama na
kuwahimiza watumishi wote kufanya kazi kwa bidii ili kukidhi matarajio
yaliyokusudiwa.
Wajumbe wa Baraza hilo pia walitoka na maazimio kadhaa
ambayo yatapelekwa kwenye Baraza Kuu la Mahakama Taifa, ikiwemo suala la
malimbikizo ya mishahara kwa watumishi na mikopo inayotolewa na hazina. Wajumbe
hao walipendekeza kila mgawo unapotolewa upelekwe kwenye vituo au Kanda za Mahakama.
Akiwasilisha taarifa yake ya utendaji kazi kwa kipindi
cha mwezi Machi 2021 hadi tarehe 27 Mei, 2022, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo,
Mhe. Magdalena Ntandu amesema Majaji na watumishi wote wanafanya kazi kwa
kujituma, ushirikiano na weledi ili kufanikisha azima yao ya kutoa haki kwa
wakati kwa wananchi.
Hata hivyo, Naibu Msajili huyo alielezea changamoto
mbalimbali katika uendeshaji wa mashauri wanazokabiliana nazo, ikiwemo kutopatikana
kwa mashahidi kwa wakati, baadhi ya mashauri kuwa na idadi kubwa ya makosa
kwenye shauri moja, idadi kubwa ya mashahidi na vielelezo, hivyo kuhitaji muda
mwingi wa kusikiliza mashauri hayo.
Changamoto nyingine ni mawakili wa Serikali kuchelewa
kufika mahakamani na kuchelewa kuandaa mashahidi, maombi ya kuahirisha shauri
mara kwa mara na washitakiwa kuchelewa kuletwa mahakamani kutokana na
changamoto ya usafiri.
Mhe. Ntandu alilieleza Baraza kuwa pamoja na
changamoto hizo, bado Divisheni hiyo ilifanikiwa katika mambo mbalimbali, ikiwemo
kupunguza kwa kiasi kikubwa na kuzuia mlundikano wa mashauri, kuendelea kusajili
mashauri kwa njia ya mfumo wa pamoja na kusikiliza baadhi ya mashauri kwa njia
ya mtandao.
Naye Mhasibu Mwandamizi Joyce Mulugu alieleza katika taarifa
yake ya mapato na matumizi ya fedha kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi
ya millioni 793 za Kitanzania zilitengwa na kupitishwa kwa ajili ya matumizi
kulingana na vipaumbele katika Mahakama hiyo.
Bi Mulugu amesema kuwa hadi kufikia Mei 2022 zaidi ya millioni
603 zimeshapokelewa kama fedha za matumizi ya kawaida na zimeshatumika
kulingana na mpango kazi, ambapo kiasi hicho ni sawa na aslimia 76 ya bajeti
nzima.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi Tumaini Mwalyoga
ameliambia Baraza alipokuwa akiwasilisha taarifa yake ya utawala na utumishi
kuwa hakuna mtumishi mwenye shauri la nidhamu au aliyechukuliwa hatua za
kinidhamu kwa kipindi cha mwaka wa fedha unaokaribia kumalizika.
Bi Mwalyoga ameahidi ofisi yake kutoa mafunzo ya ndani
kwa watumishi au kuwa na programu za kubadilishana uzoefu pale itakapowezekana
na pia watumishi watashiriki kwenye mikutano ya kitaaluma ili kuwajengea uwezo
na kupata uzoefu kwenye taasisi zingine za Serikali.
Afisa Utumishi Tumaini Mwalyoga akiwasilisha taarifa ya ofisi yake kwenye kikao cha Baraza hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni