Jumatatu, 30 Mei 2022

MSAJILI MKUU MAHAKAMA AWATAKA WAKUU WA MAENEO YA KIMKAKATI KUSIMAMIA MIRADI KWA WELEDI

Na Tiganya Vincent, Mahakama

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka Wamiliki wa maeneo ya kimkakati ndani ya Mhimili huo (SO-Owners) kuhakikisha wanatumia mafunzo ya usimamizi wa miradi kubaini na kudhibiti matukio yanayoweza kutokea na kuathiri utekelezaji wa miradi ya Mahakama inayoendelea.

Akizungumza leo tarehe 30 Mei, 2022 wakati akifungua mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili yanayofanyika Mjini Mombasa, Mhe. Chuma amesema Wakuu hao wanapaswa kutumia fursa mafunzo hayo kuongeza maarifa na weledi wa kusimamia miradi ya Mahakama inayoendelea na inayotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.

Amesema kuwa, ikiwa Wasimamizi wa Miradi inayoendelea na ile itakayoanza wakishindwa kusimamia kwa umakini na weledi wataigharimu Serikali kwa kuwa ni mkopo ambao utapaswa kulipwa kama kawaida.

“Eneo lingine ambalo mnapaswa kujifunza kwa weledi na umakini ni pamoja na namna bora ya kufanya manunuzi na kusimamia mikataba yaani (proper procurement and contract management),” amesema Msajili Mkuu.

Amesisitiza kuwa, eneo la manunuzi ni la kuangalia kwa makini na ni vema likawa sehemu ya ufuatiliaji na tathmini inayofanywa mara kwa mara kuhusu miradi husika ili kuhakikisha matokeo ya kazi yanalingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Ameongeza kuwa, ana imani mafunzo hayo yatasaidia kuwaongezea ustadi wa kusimamia miradi ya Mahakama na hatimaye kuleta tija katika Mhimili wa Mahakama na Taifa kwa ujumla.

“Nina imani kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu katika kueneza ujuzi watakaoupata kwa watumishi wengine kwa ajili kujifunza kutoka kwao  namna bora ya kusimamia miradi,” ameeleza.

Aidha, Mhe. Chuma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali kwa Watumishi wa Mahakama ya kupatiwa mafunzo.

Ameongeza pia kwa kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kukubali kuwa watumishi wapewe mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kusimamia miradi inayoendelea.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesema mafunzo hayo yametolewa kwa makundi mawili kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kusimamia kwa umakini na weledi miradi yote ya Mahakama ya Tanzania inayoendelea.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe.Wilbert Chuma (katikati) akifungua mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili ambayo yameanza leo tarehe 30 Mei, 2022 Mjini Mombasa. Wengine katika picha kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Sharmillah Sarwatt na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.

Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (aliyesimama) akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma (katikati ) kwa ajili ya kufungua mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili ambayo yameanza leo tarehe 30 Mei, 2022 Mjini Mombasa. 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya Pamoja na Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo vya Mahakama ya Tanzania baada ya kufungua mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili ambayo yameanza leo tarehe 30 Mei, 2022 Mjini Mombasa. Wengine katika picha ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia) na  Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (kushoto).

 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe.Wilbert Chuma (katikati walioka) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo vya Mahakama ya Tanzania baada ya kufungua mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili ambayo yameanza leo tarehe 30 Mei, 2022 Mjini Mombasa. Wengine katika picha ni Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia) na  Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (kushoto).

   

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni