Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma
Kaimu Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi amewaomba na
kuwasisitiza Wahasibu na Wakaguzi wa ndani kuzingatia malengo ya mafunzo kwa
vitendo watakaporudi vituoni kutekeleza majukumu yao.
Akifungua rasmi mafunzo Wahasibu na Wakaguzi wa ndani leo tarehe 30, Mei 2022 katika Ukumbi wa
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Mambi amesema mafunzo hayo ni
muhimu kama sehemu ya utekelezaji wa sera, sheria zinazosimamia masuala ya
fedha na hususani katika kipindi hiki ambacho Mahakama ya Tanzania inatekeleza Mpango
Mkakati wa Awamu ya pili wa 2020/21 hadi 2024/2025.
“Wahasibu na Wakaguzi wa
ndani wote ninyi ndiyo wasimamizi wakuu wa kusimamia namna bora ya matumizi ya fedha ama
nidhamu ya pesa za Umma, kwa lugha nyingine nyie ni wasaidizi wa Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG)”. amesema Jaji Mambi.
Mhe. Mambi, amesema kuwa, anaamini kuwa, kila
mshiriki anatambua sera, miongozo na sheria zinazosimamia
matumizi bora ya fedha za umma. Hivyo, anaamini kwamba, kupitia mafunzo hayo Maafisa hayo watajengewa uwezo, kukumbushwa
majukumu yao na kubadilishana uzoefu wa utendaji wa kila siku.
Kwa upande wa usimamizi
wa rasilimali fedha, Jaji Mambi aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa
shughuli nyingi za Serikali hasa za usimamizi wa fedha zinafanyika kwa njia ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imerahisisha kuongezeka
kwa nidhamu, uwazi, uwajibikaji na utambuzi wa matumizi usiofichika. “Natambua
mifumo hii mnaitumia kila siku katika kazi zenu ni rai yangu kwenu mzidi
kujiimarisha katika kuitumia ili kutatua changamoto mnazokabiliana nazo”,
alisisitiza Jaji Mambi.
Akifafanua kuhusu Sheria ya mtandao inayotumiwa na Wahasibu, Jaji Mambi amesema, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki
namba 13 ya mwaka 2015 inaelekeza masuala mbalimbali ikiwemo malipo ya fedha
kielekroniki, usimamizi wa fedha na pia utekelezaji wa sheria ya miamala ya
kielektroniki. Sheria tajwa kifungu cha 13 na 15 ni vifungu vya muhimu sana
katika utekelezaji wa majukumu ya kiuhasibu hasa wanapofanya malipo kimtandao.
Kifungu cha 13 cha sheria ya miamala ya kielektroniki namba 13 ya mwaka 2015 kinazungumzia zaidi serikali mtandao, kinatambua matumizi ya serikali mtandao ama huduma za serikali mtandaoni (E-Government). Kifungu cha 15 cha sheria hiyo kinaelezea malipo na uwasilishaji wa stakabadhi kielektroniki na hayo mambo ni ya msingi katika utekelezaji wa shughuli za kihasibu, aliongeza Dkt. Mambi
Washiriki wa mafunzo hayo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wameombwa kutosita kusambaza elimu waliyoipata kwa watumishi wengine ambao hawakupata nafasi hiyo adhimu ya kushiriki ili kuwajengea uwezo na uelewa wa pamoja katika kusukuma gurudumu la shughuli za Taasisi.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi (katikati) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani (hawapo katika picha) leo tarehe 30, Mei 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma. Amesisistiza uwazi, nidhamu na uwajibikaji katika kuwahudumia wananchi, wengine ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Bernard Mpepo (kulia) na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya Wahasibu na wakaguzi wa ndani wa Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Mwezeshaji (hayupo katika picha) leo tarehe 30, Mei 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni