Na Rosena Suka - Lushoto
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Katiba na Sheria, Mhe. Mary Makondo ametoa pongezi kwa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto kwa kuwa miongoni mwa taasisi chache zinazoongoza nchini
kuendesha mafunzo kwa njia ya Mtandao.
Ametoa kauli hiyo leo
tarehe 5 Mei, 2022 Jijini Dar es Salaam katika Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa
Vitendo katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo ambapo amesema Chuo
kimekuwa kikifanya vizuri kwenye eneo la mafunzo kwa njia ya mtandao sio tu
nchini bali pia katika ukanda wa Afrika na nje ya mipaka ya Afrika.
Mhe. Makondo alieleza
kwamba katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambapo matumizi ya
TEHAMA na Akili Bandia yamezidi kushika kasi, hali hiyo imetokana na ukweli
kuwa Mahakama ya Tanzania ni Mhimili unaofanya vizuri kwenye matumizi ya TEHAMA
katika utendaji kazi wa kila siku ikiwemo uendeshaji wa mashauri.
Aliendelea kusema kuwa
Chuo kama wakala wa mafunzo kwa kutumia TEHAMA kupitia mfumo wa virtualcourt
umeweza kuendesha mafunzo kwa zaidi ya watumishi 1500 wa mahakama ya Tanzania
mpaka sasa na idadi hiyo inaendelea kuongezeka. Amesema njia hiyo imeweza
kukisaidia Chuo kuwafikia watumishi wa Mahakama popote walipo bila usumbufu wa
kusafiri ambapo njia hiyo imeweza kupunguza gharama za kuwalipa watumishi kwa
ajili ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali.
Mhe.Makondo
ameonyesha kufarijika kwa jitihada
zinazofanywa na chuo cha uongozi wa mahakama kwa kuendesha mashauri na mafunzo
mbalimbali kwa kutumia mifumo ya Tehama iliyotengenezwa na wataalamu wa ndani.
"Nimefarijika sana
kuona chuo kimetumia mfumo uliojengwa na watalaamu wetu badala ya kutumia
mifumo kama Microft teams , zoom hii inatuhakikishia usalama wa mifumo pamoja
na kujenga uwezo wa ndani ,nitoe rai kwa chuo kuharakisha kuanzisha mafunzo ya
muda mfupi ya komputa kwa wanasheria" alisema Makondo.
Aidha Mhe.Makondo
amewataka wajumbe walioteuliwa katika Baraza la wafanya kazi kuhakikisha
wanakuwa mabalozi wazuri kwa wafanyakazi wanaowawakilishi na siyo kuwa mizigo
kwa uongozi na wafanyakazi katika kutatua kero zao.
Aidha Mhe. Makondo
ameupongeza uongozi wa Chuo kwa jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi
kwa kununua viwanja jijini Mwanza na Mkoani Simiyu na kusema kufanya hivyo ni
hatua kubwa kwa Chuo. "Wizara inaamini kwamba uendelezaji wa viwanja hivyo
utafanyika kwa haraka ili kufikisha huduma karibu na wananchi kama
ilivyokusudiwa,"alisema.
Mhe. Makondo ameahidi
kuwa Wizara anayoiongoza iko tayari kutoa ushirikiano unaostahili kwa Chuo
wakati wowote watakapouhitaji. Alitumia hafla hiyo kutoa wito kwa waajiri wote
wanaoajiri wanasheria katika utumishi wa umma kuwapeleka watumishi hao kupata
mafunzo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa mujibu wa matakwa ya Waraka
wa Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Waraka Namba 5
wa mwaka 2012.
Kwa upande wake Jaji wa
Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi Mhe.Dkt. Paul Kihwelo
amesema kuwa kwa kanuni ya 108 ya sheria za utumishi wa umma 2003 kanuni
zinaelekeza kuwepo kwa chombo ambacho kitahakikisha kuwepo kwa mahusiano mazuri
kazini pamoja na kuhakisha masilahi ya watumishi yanazingatiwa kwa mjibu wa
sheria.
Mhe. Dkt. Kihwelo
aliendelea kusema kuwa wajibu wa Chuo ni kuwajengea uwezo watumishi wa mahakama
kwa kada mbalimbali Tanzania ili kuboresha utendaji wa kazi kwa maafisa.
Hafla hiyo ya uzinduzi
ilikamilika kwa wajumbe kupewa mafunzo ya siku moja ya Haki na Wajibu wa
Mtumishi wa Umma pamoja na Maadili ya Utumishi wa Umma mafunzo ambayo
yameendeshwa na wawezeshaji wabobezi kutoka Ofisi ya Raisi Menejimenti ya
Utumishi ya Umma.
Lengo la mafunzo hayo
ni kuleta tija kwa watumishi, taasisi na taifa ili kuweza kukabiliana na
changamoto zitakazojitokeza katika utumishi wa mma kwa kuwa Baraza la
wafanyakazi ni kioo na mwanga wa taasisi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Mary Makondo akipokea zawadi kutoka
kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Sheria
kwa Vitendo, Mhe. Dr. Benhajj S. Masoud katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo.
Mkuu
wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akipokea zawadi kutoka kwa Jaji
wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Sheria kwa Vitendo, Mhe. Dr.
Benhajj S. Masoud katika
hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Mary Makondo akipokea zawadi ya Tisheti
kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Mwenyekiti wa Baraza
la Wafanyakazi Mhe. Dkt. Paul Kihwelo katika hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo.
Wajumbe wa Baraza Jipya la Wafanyakazi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni