Na Faustine Kapama-Mahakama, Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka
watumishi wote kokote walipo kujipa nafasi ya kufanya mazoezi na kupenda
michezo, kwani michezo ni furaha, afya na njia bora ya kujenga mahusiano mazuri
na kukutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Prof. Ole Gabriel ametoa wito huo leo tarehe 6 Mei, 2022 katika
ukumbi wa Maktaba wa Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa
vikombe viwili vya ushindi na Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) iliyovinyakua
kwenye mchezo wa kuvuta kamba kwenye mashindano ya Mei Mosi yaliyomalizika hivi
karibuni jijini Dodoma.
“Niombe viongozi wenzangu popote walipo, wasihesabu michezo kama
kupoteza muda. (Wanamichezo) wanaenda kujenga afya zao na afya ya Mahakama vile
vile. Michezo ni njia pia ya kuhamasisha watumishi kufanya kazi vizuri, michezo
ndiyo kitu pekee cha kuwaunganisha watu, hivyo kushiriki katika michezo ni
jambo zuri (na) inatujenga sana katika utendaji kazi,” amesema.
Mtendaji Mkuu, ambaye aliambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Shamillar
Sarwatt, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus
Uiso, ambaye pia ni mlezi wa Timu hiyo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na
Utawala, Bi Beatrice Patrick na Mkurugenzi Msaidizi Utawala, Bw. Stephen Magoha
amewapongeza wachezaji wote kwa kuiheshimisha Mahakama kufuatia ushindi
walioupata.
“Kuweza kuwa mshindi wa pili siyo jambo dogo, ni jambo kubwa sana.
Naungana Msajili Mkuu kuwapongeza sana, mafanikio haya siyo ya kwenu pekee
yenu, bali pia ni mafanikio ya Mahakama. Ni heshima kubwa sana ambayo
mmetupatia na kwa muktadha huo mpokee pia salamu za pongezi kutoka kwa viongozi
wetu wakuu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani,” alisema.
Prof. Ole Gabriel aliaahidi kushughulikia changamoto kadhaa
zinazoikabili Mahakama Sports, ikiwemo kutenga muda wa kufanya mazoezi, kuanza
maandalizi mapema, kununua vifaa vya michezo na amekubali ombi la timu kukaa
kambini kwa wiki moja ili kujiandaa vizuri kabla ya mashindano.
“Tutaanza mapema maandalizi ya Shimiwi na mimi naamini mtashinda. Msiwe
na wasiwasi, sijui viatu, track suit, hivi havitatushinda. Mahakama tunaendelea
kujiandaa, hii tasnia ya michezo hatuifanyii ajizi, tunamaanisha. Tutaendelea
kutenda haki katika mnyororo wa haki na pia kutenda haki katika michezo kwa
kucheza vizuri na tutashinda kwa haki kwa sababu sisi ni watu wa haki,”amesema.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, pamoja na
mambo mengine, aliwapongeza wachezaji kwa hatua waliyofikia na kwa kushiriki katika
michezo kikamilifu kwa kuzingatia kuwa siyo tu michezo ni afya bali pia inaleta
umoja na upendo.
Aidha, Mhe. Chuma aliwashauri viongozi wa Mahakama Sports kuimarisha
timu kwenye Kanda mbalimbali za Mahakama ili kupata washiriki wengi katika
michezo, hivyo kurahisisha upatikananji wa timu bora, yenye nguvu na ushindani
wa kutosha katika mashindano yajayo.
Naye Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede aliushukuru uongozi
wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwawezesha kushiriki katika mashindano hayo.
Alimwomba Mtendaji Mkuu kuendelea kuwaunga mkono ili waweze kutengeneza timu
imara kwani wachezaji wengi wazuri wapo mikoani.
“Wachezaji wapo wengi mikoani, lakini tunashindwa kuwafikia,
tukiwafikia sisi viongozi tutapata wachezaji wazuri kwenye michezo ya kuvuta
kamba, mpira wa miguu na mpira wa pete. Tumekaa muda mrefu bila kushiriki
katika mshindano haya, hivyo ni kama timu tunaijenga upya. Tunaahidi kutengeneza
timu nzuri yenye ushindani mkubwa kama unavyohitaji. Kocha tuliyenaye ni mzuri,
ana uwezo wa kututengenezea timu nzuri,” alisema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya mashindano hayo, Katibu Mkuu wa
Mahakama Sports Robert Tende alimweleza Mtendaji Mkuu baadhi ya changamoto
zinazowakabili ikiwemo kutopata muda wa kutosha kuandaa timu kwa kuwaita
wachezaji mikoani kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mazoezi ya pamoja na kufanya
mchujo ili kupata wawakilishi.
Changamoto nyingine ni uhaba wa vifaa vya michezo kama vile koni,
viatu, jezi na mabegi ya kuhifadhia vifaa. Pia alisema kuwa kumekuwepo na
uchache wa wachezaji kushiriki katika kila mchezo, hivyo kupelekea kama akitokea majeruhi kushindwa kubadili
mchezaji.
Mashindano ya Mei Mosi yaliyokuwa yanafanyika katika Uwanja wa
Jamhuri jijini Dodoma yalikamilika tarehe 29 Aprili, 2022 kwa Mahakama Sports kushika
nafasi ya pili kwenye mchezo wa kuvuta kamba wanaume na wanawake.
Mahakama Sports iliingia fainali kupambana na timu ya Uchukuzi kwa
upande wa wanaume na wanawake, lakini ikashindwa kwa taabu na wapinzani wao,
hivyo kuweza kujinyakulia vikombe viwili baada ya kushika nafasi ya pili.
Mashujaa hao wa Mahakama Sports wanawake walioshiriki katika
mashindano hayo wakiongozwa na mama Mchawi Mwanansolo walikuwa Stephania
Bishobe, Zahara Selemani, Rebecca Mwakabuba, Hadija Mkuvi, Beatrice Dibogo,
Jamila Kisusu, Judith Sarakikya, Saraphina Mkumbo, Melina Mwinuka, Namweta
Mcharo, Mwanabibi Bakari, Lucy Mbwaga, Zuhura Hamza, Scholastica Shemtoi, Josephine Aidani, Julieth Musiza na Gatty Martin.
Kwa upande wa Mahakama Sports wanaume chini ya Rajab
Mwariko walikuwa Leonard Kazimzuri, Cletus Yuda, Seleman Dimoso, Patrick
Nundwe, Denis Chipeta, Frank Lutego, Ashel Chaula, Abdul Mbaraka, Mushi Martin,
Moris Magogo, Chilemba Chikawe, Issa Kabandika, Philipo Ferdinand, Emmanuel
Seshahu na Fred Ndimbo.
Mahakama Sports iliingia robo fainali baada ya kushinda mechi zake
zote kwenye hatua ya makundi. Mahakama Sports wanaume walimenyana na TPDC na
Tanesco, ambao waliingia mitini kwa kuhofia kipigo, huku Mahakama Sports
wanawake ikiwazalisha Ocean Road, Tanesco na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Baada
ya hapo, Mahakama Sports ilikutana na TPDC kwenye nusu fainali na kufanikiwa
kutinga fainali kukutana na Uchukuzi.
Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede (wa tatu kulia) akikabidhi kombe kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, huku Katibu wa Mahakama Sports Robert Tende (wa pili kushoto) akimkabidhi kombe Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni