·Mkuu wa Wilaya atangaza msako waliohusika
Na Ahmed Mbilinyi- Mahakama, Bukoba
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera, Mhe. Toba
Nguvila ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama katika Wilaya hiyo kuwakamata
na kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaodaiwa kuchoma moto gari la Hakimu wa
Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda wilayani humo, Mhe Emmanuel Sheiza nyumbani kwake.
Mhe. Nguvila alitoa agizo hilo jana tarehe 9Mei,
2022 alipotembelea eneo la tukio na baadaye kuongea na wanakijiji wa kitongoji
cha Nyamilanda na kuelezea masikitiko yake makubwa. Tukio hilo limetokea usiku
wa kuamkia jana ambapo watu wasiofahamika walichoma moto gari la Hakimu huyo.
Mkuu wa Wilaya huyo amesema, “Tayari tukio hili la
kusikitisha limesharipotiwa katika vyombo vya ulinzi na usalama na uchunguzi unaendelea
ili kuwakamata wahusika wote na hakuna hata mmoja atakayekwepa mkono wa chuma
wa sheria.” Hakimu huyo anaishi kwenye nyumba za Mahakama zilizopo jirani na
Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda.
Mhe Nguvila amemuhakikishia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Bukoba, Mhe. Dkt Ntemi Kilekamajenga,
ambaye aliambatana na viongozi wengine wa Mahakama kufika katika eneo la tukio ili kumpa pole Mhe Sheiza kwa janga hilo kuwa wote walihusika watapatikana na
kuchukukiwa hatua kali.
Viongozi wengine wa Mahakama walioambatana na Mhe. Kilekamajenga
walikuwa Msajili wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, Mhe. Amoro Odira, Hakimu
Mfawadhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Mhe Janeth Massesa, Hakimu
Mfawadhi wa Mahakama ya Wilaya Muleba, Mhe Asha Mwetindwa na Mtendaji wa Mahakama
Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko.
Gari la Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda, Mhe
Emmanuel Sheiza likiwa limeteketea kabisa kwa moto baada ya kuchomwa na watu
wasiofahamika.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nyamilanda, Mhe
Emmanuel Sheiza (mwenye suti ya blue) akimuonyesha Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe.
Dkt Ntemi Kilekamajenga jinsi tukio lilivyotokea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia
ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe Toba Nguvila (wa tatu kulia) akimpa pole Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe Ntemi Kilekamajenga (katikati) kwa tukio hilo.
Amemuhakikishia kuwa wahusika wote walioshiriki katika tukio hilo watakamatwa
na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni