Jumanne, 10 Mei 2022

TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA KUTUMIA MFUMO WA KIELEKITRONIKI KWENYE MICHAKATO YA AJIRA

Na Lydia Churi- Morogoro

Tume ya Utumishi wa Mahakama inakusudia kuanza kutumia mfumo wa Kielekitroniki (Ajira Portal) kwenye michakato ya ajira za watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kuendana na mabadiliko ya Teknolojia pamoja na kuongeza ufanisi.

Akiwasilisha Mada kwenye Mafunzo kwa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama yaliyohudhuriwa pia na Watendaji kutoka Sekretarieti ya Ajira nchini kuhusu Mfumo huo mkoani Morogoro, Naibu Katibu wa Tume hiyo Bi. Enziel Mtei alisema kuwa Tume imeamua kuhama kutoka kwenye mfumo wa ajira wa sasa kwenda kwenye mfumo wa kielekitroniki kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuokoa muda mrefu unaotumika katika mchakato wa ajira

Naibu Katibu huyo pia alitaja sababu za Tume hiyo kutumia mfumo wa kielekitroniki kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za matumizi ya shajala kama vile karatasi, wino na vifaa vingine vya ofisi vinavyotumika wakati wa mchakato huo kutokana na idadi kubwa ya waombaji ya ajira pindi Tume hiyo inapotangaza nafasi za kazi.

“Sababu nyingine iliyoifanya Tume ya Utumishi wa Mahakama kutaka kuingia kwenye matumizi ya mfumo wa kielekitroniki katika kupata watumishi wake ni kutokana na faida za mfumo huu ambao hautumii idadi kubwa ya Rasilimaliwatu” alisema Naibu Katibu.

Alifafanua kuwa mfumo unaotumika hivi sasa hutumia idadi kubwa ya watumishi huku akitolea mfano wa idadi kubwa ya watumishi wa Tume hutumika kufanya kazi kama vile kubeba barua za maombi kutoka Posta, kufungua barua hizo, kuorodhesha kwenye rejesta, kupiga mihuri, kuingiza kwenye kompyuta na kuhakiki taarifa za waombaji wa ajira zilizorekodiwa.

Katika kujiandaa kuingia kwenye matumizi ya mfumo wa kielekitroniki, Bi. Mtei alisema kuwa tayari Tume imetenga fedha katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya maandalizi ya matumizi kutekeleza nia yake ya kuachana na mfumo wa sasa unaotumika katika mchakato wa ajira za watumishi wa Mahakama.

Alisema lengo la kukutana na watendaji wa Sekretarieti ya Ajira ni kupata uzoefu wao namna mfumo wa “Ajira Portal” unavyofanya kazi hasa ukizingatia kuwa wao wameanza kuutumia kwa muda mrefu.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 113 (4), Tume ya Utumishi wa Mahakama imepewa jukumu la kuajiri watumishi wa Mahakama wa kada ya Mahakimu. Aidha, kifungu cha 29 (1) (e) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 kinaipa Tume hiyo jukumu la kuajiri watumishi wa Mahakama wasio Mahakimu wa ngazi zote.

 

Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Enziel Mtei (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi Watumishi wa Tume hiyo pamoja na Baadhi ya Maafisa Tehama wa Sekretariet ya Ajira mara baada ya kuanza mafunzo kuhusu Mfumo wa Kielekitroniki wa Mchakato wa Ajira. Wa tatu kushoto ni Naibu Katibu wa Idara ya Menejimenti ya Ajira kutoka Secretariet ya Ajira Bw. Lucas Mrumapili. 


Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Enziel Mtei akizungumza wakati wa mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Morogoro. 
Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Sekretariet ya Ajira wakiwa kwenye mafunzo hayo. Watumishi kutoka Secretariet ya Ajira wanahudhuria mafunzo hayo kwa lengo la kutoa uzoefu kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhusu Ajira Portal.

Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Sekretariet ya Ajira wakiwa kwenye mafunzo hayo. Watumishi kutoka Secretariet ya Ajira wanahudhuria mafunzo hayo kwa lengo la kutoa uzoefu kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuhusu Ajira Portal.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni