Na Francisca Swai-Mahakama, Musoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe
10 Mei, 2022 alifanya ziara ya kikazi ya siku moja ya Mahakama Kanda ya Musoma na kuwapongeza watumishi kwa
utandaji kazi bora katika kutekeleza majukumu mbalimbali.
Katika ziara yake, Prof. Ole Gabriel
alikagua miradi ya ujenzi unaoendelea wa Mahakama za Wilaya Rorya na Butiama
ambayo ipo chini ya Mkandarasi United Builders Limited na Mshauri HY Projects
Consultant Limited na kuhimiza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kupongeza ubora wa kazi
inayoendelea.
Mtendaji Mkuu hakuridhishwa na kasi ya
ujenzi wa miradi hiyo iliyotakiwa kukamilika tangu tarehe 12 Aprili, 2022, hivyo
aliumsisitiza Mkandarasi kuongeza nguvu kazi pamoja na usimamizi ili miradi
hiyo iwe imekamilika kufikia mwishoni mwa mwezi Mei 2022.
Baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mtendaji Mkuu alipata nafasi ya kukagua jengo
la Mahakama Kuu Musoma pamoja na kuongea na viongozi na watumishi wa Mahakama hiyo,
Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo
Musoma Mjini katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Musoma (Open Court).
Katika kikao na watumishi hao, Prof. Ole
Gabriel aliwapongeza watumishi wa Kanda ya Musoma kwa utendaji kazi wao mzuri
ambao aliuelezea kuwa ni wa kuigwa pamoja na jitihada wanazofanya kulitunza
jengo la Mahakama Kuu na mazingira yake kwa ujumla.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo aliahidi
kushughulikia changamoto mbalimbali zilizowasilishwa kwake na uongozi wa Kanda
ya Musoma pamoja na watumishi zikiwemo, ujenzi wa uzio wa Mahakama ya Mwanzo
Robanda, ujenzi wa Kanteeni kwa ajili ya huduma ya chakula kwa watumishi, wadau
na wateja wa Mahakama Kuu Musoma na upatikanaji wa gari la ziada kwa ajili ya
shughuli za kiofisi pamoja na basi la watumishi.
Prof. Ole Gabriel aliwaasa watumishi
kupendana na kuzipenda kazi zao, kujiendeleza kitaaluma ikiwezekana kupanua
wigo nje ya taaluma zao za sasa.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amemshukuru Mtendaji Mkuu kwa ujio wake katika
Kanda hiyo na kumhakikishia kuwa maelekezo
aliyoyatoa yanayotekelezeka yatafanyiwa kazi.
Kaimu
Mtendaji Kanda ya Musoma Bi, Alicia Felician (katikati) akielezea jambo wakati
wa ukaguzi wa jengo na mazingira ya Mahakama Kuu Musoma.
Afisa
TEHAMA Kanda ya Musoma Bw. Simon Lyova (mwenye tai nyeusi) akielezea jambo kwa Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa ukaguzi wa
mifumo ya TEHAMA inayotumika katika jengo la Mahakama Kuu Musoma.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akishauriana jambo na
Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Rorya, Eng. Pius Mallya kuhusu
mpango kazi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Rorya.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akielekeza jambo kwa
Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Rorya baada ya ukaguzi wa
mradi huo.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua ubora wa
mchanga unaotumika katika upigaji lipu kwenye jengo la Mahakama ya Wilaya
Butiama.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole akiongea na wasimamizi wa
mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Butiama wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya
ujenzi wa mradi huo.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na watumishi
wa Kanda ya Musoma wakati wa ziara yake katika Kanda hiyo.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya
pamoja na viongozi na watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni