Alhamisi, 26 Mei 2022

JAJI KIONGOZI MAHAKAMA KUU YA TANZANIA YUPO KANDA YA SUMBAWANGA

·Kumuaga kitaaluma Jaji Mrango leo

·Atoa wito maalumu kwa Mahakimu

Na. James Kapele  na Mayanga Someke– Mahakama ,Sumbawanga

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 26 Mei, 2022 amewasili katika Kanda ya Sumbawanga kwa lengo la kushiriki kumuaga kitaaluma Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. David Mrango ambaye amestaafu.

Shughuli  hiyo maalumu inatarajiwa kufanyika kesho katika jengo la Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga ambapo Mhe. Siyani atakuwa kiongozi mkuu.

Akiwa njiani kuelekea Sumbawanga mjini, Jaji Kiongozi amepata fursa ya kutembelea Mahakama za Mwanzo mbili za Laela na Mpui ambapo, pamoja na mambo mengine, ametoa maelekezo mbalimbali kwa Mahakimu kumaliza mashauri kwa wakati pamoja na kuzingatia maadili ya watumishi.

Akiongea baada ya kuwasili katika Mahakama ya Mwanzo Laela na baadaye kupokea taarifa ya hali ya mashauri mahakamani hapo, Mhe. Siyani amewasihi watumishi na viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili kwa kuwa ndiyo yanayobeba taswira ya Mahakama.

“Nyinyi watumishi wa Mahakama hapa Laela mnabeba taswira ya Mhakama ya Tanzania nzima, mkiwahudumia wananchi  vibaya wanaona Mahakama yote Tanzania ni mbaya, hivyo wahudumieni wananchi vizuri kwa kuwa Mahakama ndiyo kimbilio lao.” alisema Mhe. Siyani.

Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi amepata fursa ya kutembelea Makakama ya mwanzo Mpui ambapo alipokea pia taarifa ya hali ya mashauri katika mahakama hiyo.

Akiwa katika Mahakama hiyo, Mhe. Siyani amewataka watumishi kufanya kazi kwa kujiwekea malengo yanayotofautiana na mahakama nyingine kwa kuzingatia uchache wa mashauri yanayofunguliwa mahakamani.

“ Kwa uchache wa haya mashauri yaliyofunguliwa katika Mahakama hii ni wazi kwamba huwezi kuendelea kusubiri shauri lifikie miezi sita kuingia kwenye mlundikano. Jiwekeeni malengo yanayotofautiana na Mahakama nyingine kwa sababu mnao muda wa kutosha kufanya kazi nyingine,” amesema.

Amewahimiza Mahakimu kumaliza mashauri hata ndani ya miezi mitatu toka kufunguliwa kwake ili wananchi waweze kufurahia huduma za Mahakama. Aidha, Jaji Kiongozi amewataka Mahakimu hao kutoa nakala za  hukumu mapema bila kusubiri siku thelathini.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania anatarajia kushiriki katika shughuli ya kumuaga kitaaluma Jaji Mrango aliyestaafu utumishi wake mwaka jana.

 



Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akisalimiana na viongozi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga. Anayesalimiana naye ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bw. Emmanuel Munda.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama wakisalimiana na Jaji Kiongozi alipowasili Mahakama ya Mwanzo Laela.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Mahakama ya Mwanzo Laela. 

 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akipanda mti wa kumbukumbu katika Mahakamya Mwanzo Laela. Aliyesimama wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru.

 


 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni