Na Mwandishi wetu-Mahakama
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke
kinachoshughulikia masuala ya kifamila, ndoa na talaka kilichopo Wilaya ya Temeke
mkoa wa Dar es Salaam kimefanikiwa kuboresha mfumo wa matangazo kwa wateja (PA
SYSTEM) ambao hutumika kuwaalika na kuwaita shaurini wadaawa wanaofika mahakamani
na kuketi kwenye maeneo mbalimbali.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 26 Mei, 2022 na Afisa TEHAMA
wa Kituo hicho, Bi. Amina Said alipokuwa akitoa mafunzo kwa watumishi wa kada mbalimbali.
Amesema kuwa hapo awali ilifungwa “Microphone” moja eneo la chini upande
wa mapokezi, ambapo ilimlazimu kila mtumishi kutoka eneo alipo ndani ya jengo lenye
ghorofa tatu kushuka chini kutangaza, hatua ambayo ilileta usumbufu na upotevu
wa muda.
“Hivi sasa mfumo mpya umeunganishwa na simu za mezani,
ambapo kila ofisi iliyofungwa simu hizo inaweza kupata huduma ya kurusha
matangazo kwa wateja. Hii imerahisisha zoezi la watumishi kuhama kutoka sehemu
moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutoa matangazo na hivyo kuokoa muda,”
amesema.
Bi. Said amewaelekeza washiriki namna ya kutumia simu
hizo ili kutofautisha mfumo wa ndani wa mawasiliano na ule wa nje ambao hupaza sauti
kwenye spika, kwani mifumo yote miwili imeunganishwa kwa pamoja.
Aliwasisitiza
watumishi hao pia kutumia lugha fasaha ya Kiswahili, kutoa salamu kwa wateja,
kuweka utangulizi wanapoanza kutoa matangazo, kutaja aina na namba ya shauri, kutaja
majina ya wahusika katika shauri pamoja na kutoitisha kesi zaidi ya mbili kwa
wakati mmoja kwa wateja wanaohudumiwa eneo moja, kwani kwa kufanya hivyo itasababisha
msongamano kwenye korido.
Msaidizi wa kumbukumbu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki – Temeke, Bi. Theresia Sheshe akifanya majaribio ya kutoa matangazo kwa wateja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni