Alhamisi, 26 Mei 2022

JAJI MFAWIDHI MOROGORO AIPALILIA SENSA YA WATU NA MAKAZI

 Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewahimiza watumishi wote wa Mahakama kwenye Kanda yake kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika nchi nzima mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza na chombo cha habari cha Imani kilichopo mkoani hapa mapema jana tarehe 25 Mei, 2022 asubuhi, Mhe. Ngwembe alisema kuwa kwa sasa nchi inaelekea kwenye tukio hilo muhimu ifikapo tarehe 23 Agosti, 2022, hivyo ni rai yake kwa watumishi kujitokeza kuhesabiwa.

“Mahakama ni sehemu ya jamii na sensa ni suala la kitaifa, hivyo tupo pamoja katika kuhimiza zoezi hili liweze kufanikiwa. Tunapotaka kusogeza huduma ya Mahakama kwa wananchi lazima tujue takwimu halisi ya watu tunaowasogezea huduma hii, wako wapi na wako kwa idadi gani. Hivyo, majibu ya maswali yote haya tutayapata kupitia sensa,” alisema.

 Aidha , Mhe. Ngwembe alielezea kuwa kujua idadi ya watu ni uchumi na pia ni suala la maendeleo ya jamii, kwani itarahisisha hata kwenye usogezaji wa huduma kwa wananchi. Aliitaja nchi ya China ambayo imefanikiwa kiuchumi baada ya kutumia idadi kubwa ya watu wanaopatikana katika nchi hiyo.

“Ni rai yangu asiwepo Mtanzania yeyote atakayesema mimi sipo tayari kuhesabiwa , bali wote tuone fahari kushiriki zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Kila mmoja ashiriki yeye na familia yake, sisi Mahakama Kanda ya Morogoro tutakuwa wa kwanza kuhesabiwa  ifikapo tarehe 23 Agosti, 2022,”  alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo.

Hii itakuwa sensa ya sita kufanyika nchini tangu uhuru. Kwa mara ya mwisho Tanzania ilifanya sensa ya watu na makazi tarehe 26 Agosti, 2012. Sensa zingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa ukoloni zilifanyika sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika sensa mara moja mwaka 1958.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akifafanua jambo alipokuwa anaongea na kituo cha habari cha Imani kilichopo mkoani Morogoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (kulia) akitolea majibu swali lililoulizwa na Mtangazaji Kassim Lyimo ( kushoto) alipokuwa katika studio ya kituo cha habari cha Imani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (kulia) akiagana na Mtangazaji wa Televisheni ya Imani, Bw. Kassim Lyimo (kushoto) mara baada ya kumaliza kipindi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni