Alhamisi, 26 Mei 2022

WITO MUHIMU WA JAJI CHABA KWA WAHITIMU MAFUNZO MOROGORO

 Na Evelina Odemba – Mahakama,  Morogoro

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba amewataka watumishi walioshiriki mafunzo kuhusu uandaaji na uratibu wa taarifa za mashauri ya rushwa kuwa mabalozi wazuri katika utoaji huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo jana tarehe 25 Mei, 2022 kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Paul Ngwembe, Jaji Chaba alisema kuwa ni matumaini ya Mahakama kwa washiriki wote zaidi ya 40 watakuwa mfano bora katika kuwahudumia wteja wao bila kusahau kuzingatia matumizi ashihi ya muda.

“Hatutegemei kuona changamoto binafsi zinaathiri utoaji huduma kwa wateja,” aliwaambia washiriki hao wa mafunzo ambayo yalilengwa kwa maafisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na wasaidizi wa kumbukumbu kutoka Mahakama za Tanzania.

Aidha, Mhe. Chaba alisiwasitiza watumishi hao kuwa matumizi ya teknolojia katika shughuli za mahakamani hayakwepeki hususani linapokuja suala la usimamizi na utoaji wa takwimu za mashauri mbalimbali yakiwemo ya rushwa na ndio maana mafunzo hayo yamewahusisha maafisa TEHAMA.

Akinukuu maneno ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyoyasema kupitia hotuba yake siku ya sheria nchini akiwa Dodoma tarehe 23 Februari, 2022 kuhusu matumizi ya TEHAMA, Jaji Chaba alisema:

“Mheshimiwa Rais, Kauli Mbiu inatutaka tusirudi nyuma katika teknolojia tuliyonayo. Tutumie Mapinduzi ya Nne ya Viwanda kwa kuiendeleza zaidi. Kwa miaka iliyobaki kabla ya tarehe 31 Desemba, 2025, ninawasihi watumishi wa Mahakama na wadau wote katika Sekta ya Sheria tuendelee kuvuna faida ya uwekezaji katika teknolojia”.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mratibu wa Programu ya Kujenga Vitendo Endelevu vya Kupambana na Rushwa nchini (BSAAT), Bw. Nkrumah Katagira alisema kuwa washiriki wamepata fulsa ya kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo utoaji huduma bora kwa wateja kwa kuzingatia matumizi mazuri ya muda wa kazi.

Kwa mujibu wa Bw. Katagira, washiriki pia wamejifunza mfumo mzima wa uandaaji na utunzaji kumbukumbu za mashauri (JSDS II) na mfumo mpya wa usimamizi wa mashauri unaotarajia kuanza kutumika mara utakapokamilika.

Aliongeza kuwa mafunzo waliyoyapata washiriki watayatumia kama chachu ya kuleta ufanisi katika majukumu yao hasa upande wa matumizi ya mfumo wa usimamizi wa mashauri.

Mshiriki toka Bukoba, Bw. Gosbert Rugaika alitoa shukurani kwa niaba ya wote na kuahidi kutumia mafunzo hayo kama muongozo katika majukumu yao ya kila siku, hivyo Mahakama itegemee kuona mabadiliko ya dhati katika uwajibikaji.

Katika kuhitimisha mafunzo hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi huyo awatunuku vyeti washiriki zaidi ya 40 waliohudhulia mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yalifanyika kupitia programu ya BSAAT ambayo yalijikita katika kujenga mfumo endelevu wa mapambano dhidi ya rushwa, hasa rushwa kubwa, mradi ambao unafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya ambapo kwa hapa nchini unaratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akizungumza na watumishi wa Mahakama wakati wa kufunga mafunzo kuhusu uandaaji na uratibu wa taarifa za mashauri ya rushwa.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza Jaji Chaba. 
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akitoa vyeti vya ushiriki kwa baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo (juu na chini).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni