Jumanne, 17 Mei 2022

JAJI MKUU PROF JUMA ASHAURI UJENZI WA MAGEREZA KURAHISISHA UONDOSHAJI WA MASHAURI

 Mary Gwera, Mahakama, Kilindi-Tanga

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa mamlaka husika kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga Magereza katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na maeneo mengine nchini yenye uhitaji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya haki kwa wakati.

Akizungumza katika siku ya pili ya ziara yake Mahakama-Kanda ya Tanga leo tarehe 17 Mei, 2022 akiwa wilayani Kilindi, Jaji Mkuu, Prof. Juma amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili Wilaya hiyo ni ukosefu wa Gereza hali inayolazimu kutumia Gereza lililopo wilayani Handeni.

“Ukizingatia umbali uliopo kati ya Handeni mpaka hapa ni mrefu, hivyo baada ya kuja hapa leo tunaelewa ugumu ambao wanapata Mahabusu hao kusafiri umbali huo na ukizingatia na hali ya magari ya Magereza, hivyo kwa kuzingatia haki za binadamu ni muhimu kulizingatia suala hili,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Aliongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho Mahakama ya Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya majengo yake ni muhimu pia wadau wa mnyororo wa haki kwenda pamoja na Mahakama ili kuboresha kwa pamoja huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa Mahakama inaangalia zaidi kuhusu haki ya mtu, hivyo ni muhimu kulichukua suala hili kwa uzito wa kipekee ukizingatia Magereza nyingi ni chakavu kwakuwa zimejengwa kipindi cha ukoloni.

Awali, akitoa taarifa ya Wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe. Abel Busalama amesema kuwa Wafungwa na Mahabusu wenye mashauri katika Mahakama wilayani humo wanapata changamoto kwakuwa umbali ni mrefu takribani kilometa 120 kutoka Handeni.

“Miongoni mwa changamoto ambazo tunakabiliana nazo ni pamoja na Wilaya hii kukosa Gereza, hali hii inaathiri haki za Mahabusu lakini pia kuongeza gharama kwa Serikali kwa kuwasafirisha Mahabusu hao,” ameeleza.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kupata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Gereza hilo. Kadhalika, Mhe. Busalama alimuomba Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma kufikiriwa katika ujenzi wa Mahakama kwakuwa Wilaya hiyo inakabiliwa pia na uhaba wa majengo ya Mahakama.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo, naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi, Mhe. John Chacha alimjuza Jaji Mkuu kuwa mlundikano wa baadhi ya mashauri unachangiwa na umbali wa gereza la Handeni kwa kuwa mahabusu hawaletwi mahakamani kwa muda mrefu hivyo kesi kutosikilizwa kwa wakati.

Mhe. Chacha alisema Mahakama hiyo ina jumla ya mashauri 24 ya muda mrefu ambapo mashauri 21 yapo juu ya mamlaka ya Mahakama ya Wilaya. Jumla ya mashauri matatu Mahakama hiyo ina mamlaka nayo, mashauri mawili (2) ya uhujumu uchumi upelelezi ulikamilika mwezi Aprili, 2022 usikilizwaji wake unaendelea na shauri moja (1) lipo kwenye hatua ya hukumu.

Katika siku ya tatu (3) ya ziara yake, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma anatarajia pia kutembelea Wilaya za Lushoto na Korogwe kabla ya kuhitimisha ziara yake Tanga mjini.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Wilaya ya Kilindi na sehemu ya Watumishi wa Mahakama wilayani huo. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor, wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Abel Busalama, wa pili kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Beda Nyaki na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza alipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi alipowasili leo tarehe 17 Mei, 2022 kwa ziara ya kikazi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati), akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe. Abel Busalama (kulia) wakati Mhe. Prof. Juma alimpomtembelea Mkuu wa Wilaya huyo ofisini kwake wilayani Kilindi.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi, Mhe. John Chacha akiwasilisha mada ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) pindi alipofika katika Mahakama hiyo kwa ziara hiyo.

Ukaguzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kilindi.

Picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya Kilindi. Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor na kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe na Watumishi wa Wilaya hiyo na baadhi ya Watumishi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor akizungumza katika kikao kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Handeni.

 Picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Handeni.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni