Na. Faustine Kapama, Mahakama, Tanga.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapa Majaji Wafawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kote nchini siku 14 kuhuisha taarifa muhimu za
mashauri kwenye Mfumo wa Kuratibu Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS-II)
ili kutekeleza azma ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao (e-Judiciary).
Mhe.
Prof. Juma ametoa agizo hilo leo tarehe 17 Mei, 2022 katika siku ya pili ya
ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga, ambapo amekutana na Wakuu wa Wilaya za Kilindi na Handeni, kukagua
ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kilindi na kuongea na watumishi katika Wilaya hizo
mbili.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kilindi, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa amepata
taarifa kuwa Mkoa wa Tanga unafanya vizuri kwenye eneo la kuhuisha taarifa kwenye
JSDS-II, lakini kwa bahati mbaya, Mahakama Kuu zingine zimeanza kushuka na
kurudi kwenye karne ya 19. Amezitaja Mahakama Kuu zinazofanya vizuri kuwa ni
Tanga, Tabora, Mwanza, Musoma, Songea na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke.
“Mwishoni
mwa mwezi huu wote tuingie kwenye ligi moja ya Tanga, Tabora, Mwanza, Musoma,
Songea na Kituo Jumushi Temeke. Hawa wote ndiyo wapo kwenye mstari, wengine
wote wameshaanza kubaki nyuma. Sasa kwenye mapinduzi haya, tukiwa wengine tunabaki
nyuma ndiyo hao hao watakaotuvuta nyuma, inabidi wafuatiliwe, pengine tuwaulize
kwa nini hawahuishi hizi taarifa,”aliagiza Jaji Mkuu.
Akiwa
katika Mahakama hiyo, Mhe. Prof. Juma pia alipokea taarifa ya utendaji
iliyowasilishwa kwake na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. John Chacha, ambaye
ameeleza kuwa Mahakama yake na Mahakama za Mwanzo zinaendelea na zoezi la
utoaji wa elimu kwa wananchi wanaofika mahakamani kuhudhuria mashauri yao kabla
ya kuanza vikao vya Mahakama kila siku.
“Katika
zoezi hilo wananchi wamepata fursa ya kufahamu taratibu mbalimbali za
uendeshaji wa shughuli za kimahakama, kufahamu sheria na taratibu mbalimbali
ambazo Mahakama inazitumia kuendesha mashauri,” Hakimu huyo alimweleza Jaji
Mkuu.
Kabla
ya kuongea na watumishi hao, Mhe. Prof. Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya ya
Kilindi, Mhe. Abel Busalama, ambaye alimweleza changamoto mbalimbali
zinazoikabili Mahakama ya Wilaya, ikiwemo uhaba wa watumishi, uchakavu wa
majengo na ukosefu wa gereza, jambo ambalo huathiri kwa kiasi kikubwa kasi ya
uondoshaji wa mashauri ya jinai.
Baadaye
Mkuu wa Wilaya hiyo alimwongoza Jaji Mkuu kukagua ujenzi wa jengo jipya la Mahakama
ya Wilaya linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya shillingi millioni 657 za
Kitanzania ambalo kwa sasa lipo tayari kutumika na litakuwa chini ya uangalizi
kwa mwaka mmoja hadi Mei 2023.
Kabla
ya kuhitimisha ziara yake leo, Mhe. Prof. Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya ya
Handeni, Mhe. Siriel Mchembe ambaye ameumwagia sifa uongozi wa Mahakama ya
Tanzania kwa kusimamia uboreshaji wa huduma za Mahakama, ikiwemo utoaji wa
elimu ya kisheria kwa wananchi na kushughulikia mashauri kwa njia ya mtandao.
Hata
hivyo, Mhe. Mchembe alimwomba Jaji Mkuu kuingangalia Wilaya yake yenye Kata 33 kwa
jicho la kipekee kwa vile ndiyo kubwa zaidi kuliko zingine mkoani Tanga na inachangamoto
kubwa ya uhaba wa majengo ya Mahakama katika ngazi za Mahakama za Mwanzo na
Mahakama ya Wilaya. Mhe. Prof. Juma alimwahidi kiongozi huyo wa Serikali kushughulikia
changamoto alizoziainisha.
Baadaye,
Mhe. Prof. Juma alipokea taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Wilaya ya Handeni
kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Munga Sabuni, ambaye aliainisha
mafanikio kadhaa yaliyofikiwa, ikiwemo kuongeza kasi ya uondoshaji wa mashauri
hadi kufikia asilimia 35 kwa Mahakama ya Wilaya na asilimia 85 kwa Mahakama za
Mwanzo.
Mafanikio
mengine ni Mahakimu kuendelea kuchapa hukumu na mienendo ya mashauri wao
wenyewe, usimamizi wa nidhamu kwa watumishi na kulipa stahiki zao kwa wakati,
kuimarisha mahusiano na wadau wa Mahakama na kusajili mashauri kimtandao,
kuhuisha taarifa katika JSDSII kwa wakati na kusajili na kuhuisha mashauri
katika ‘Primary Court App’ kwa asilimia 87.
Katika
siku ya tatu ya ziara yake, Jaji Mkuu anatarajia pia kutembelea maeneo mbalimbali
ya Lushoto na Korogwe kabla ya kuhitimisha ziara yake Tanga mjini. Mhe. Prof. Juma ameongozana na viongozi
mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Kevin Mhina, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama,
Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba.
Wengine
ni Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi
Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory
Kagaruki, mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes
Mombury, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Bw. Yohana Mashausi, Afisa Utumishi, Bw.
Jeofrey Mnemba, Mpima Ramani Abdallah Nalicho, Mhandisi Peter Mrosso na
Msaidizi wa Sheria wa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Hassan Chuka.
Kwa
upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa
Mansoor, Naibu Msajili Beda Nyaki, Mtendaji Humphrey Paya, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Sofia Masati, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Mhe. Ruth Mkusi na Msaidizi wa Sheria wa
Jaji Mfawidhi, Mhe. Grace Mwaikono.
Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba (juu) na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory Kagaruki (chini) wakijibu baadhi ya hoja hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni