Jumanne, 17 Mei 2022

MDEE NA WENZAKE KUENDELEA KUWA WABUNGE HADI MAHAKAMA ITAKAPOSIKILIZA NA KUAMUA

 

 Na Magreth Kinabo – Mahakama

Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu, Mei 12 mwaka huu ilipokea kesi ya madai namba 16 ya mwaka 2022 kati ya Mdee na wenzake 18 dhidi ya Bodi ya Udhamini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kesi hiyo ya madai Mdee na wenzake waliomba ruhusa ya Mahakama ili iweze kufungua shauri la kupitia upya uamuzi wa CHADEMA wa Mei 11, mwaka huu kuhusu kufukuzwa uanachama wao. Shauri hilo limepangwa mbele ya Jaji John Samwel Mgetta, ambapo lilipangwa kutajwa Juni 16, mwaka huu saa 4.00 asubuhi.

Wakati huohuo mara baada ya kufungua shauri hilo, walifungua shauri dogo la maombi namba 13 la mwaka 2022, wakiomba zuio la muda dhidi ya NEC na AG kubatilisha nafasi zao kama wabunge wa viti maalum wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine.

Mahakama hiyo imekubali kutoa zuio la muda kuhusu ubunge wa Halima Mdee na wenzake, ambapo wataendelea na nafasi zao za wabunge wa viti maalum wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha 2020 hadi 2025 mpaka shauri lao litakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mahakama hiyo jana ilitoa wito kwa waombaji na wajibu maombi kufika mahakamani 8.00 mchana, ambapo wote walifika kwa wakati.


Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania.

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni