Na Mwandishi wetu
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani hivi karibuni aliongoza
viongozi mbalimbali wa Mahakama kumuaga kitaaluma Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Wilbard Mashauri.
Akizungumza katika
sherehe hizo zilizofanyika viwanja vya Mahakama Kuu Mwanza, Mhe. Siyani alimwelezea
Jaji mstaafu Mashauri kuwa mtu makini na madhubuti katika masuala nyeti na alisimama
kama mtu mwenye mtazamo huru, alimsikiliza kila mtu na hakuwa na uvumilivu na
watu wasiokuwa na uadilifu.
Jaji Kiongozi alitoa
mfano wa shauri la rufaa namba 1/2021- kati ya Eliada Phinias Machumu dhidi ya Christian
Mau, ambalo lilikuwa limesheheni udanganyifu uliokuwa umetengenezwa kwa umahili
wa hali ya juu, ambapo mume wa mrufani aliuza nyumba na akampa talaka mrufani.
“Mara baada ya kuuza nyumba
alifungua shauri katika Baraza la Ardhi la Wilaya akidai nyumba hiyo kwa
kutumia jina la mtalaka wake (mrufani) ambapo alishindwa na kuleta rufaa Mahakama
Kuu ndipo mrufani(mtalaka) alipata taarifa na kuiandikia barua Mahakama na
kueleza kuwa hakuwahi kufungua shauri lolote bali ni udanganyifu umefanyika kwa
kughushiwa saini yake na mtalaka wake akiwa na nia ya kupora nyumba ambayo
alikuwa ameiuza,” alieleza Mhe. Siyani.
Pia Jaji Kiongozi
alieleza kuwa Mhe. Mashauri alikuwa makini na ujanja wa mawakili ambao walikuwa
na tabia ya kuzuia upatikani wa haki kwa wakati kwani hakuwapa nafasi na hali
hiyo iliweza kuthibitishwa pia katika shauri la Omega Fish Ltd dhidi ya Zakayo
Kabali, Maombi namba 91/2018, hivyo alitamani mashauri yote yaendeshwe kwa
mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Jaji
mstaafu Mashauri alisema kuwa katika utendaji kazi wake hawezi kusau shauri
alilopangiwa kuliendesha baada ya kuhamishiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
lililokuwa linawahusu viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kwani ni shauri lililokuwa na changamoto nyingi, ikiwemo ukosoaji na tuhuma
nyingi kuwa hakuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Alieleza kuwa wakosoaji
wake walikuwa wakidai kuwa alikuwa akifanya kazi kwa shinikizo la watu ambao
hawakuweza kutajwa na mara nyingi alitishiwa kuuawa baada ya kukataa kujitoa
katika shauri hilo, msukumo ambao haukutoka kwa watu wa mbali tu bali hata
baadhi ya watu wake wa karibu walimuomba ajitoe.
Baadhi ya Majaji
wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria sherehe hizo ni Majaji wote
wa Mahakama Kuu Mwanza, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma na
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Sherehe hizo za kumuga
zilianza kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bw. Mamti kuiomba Mahakama iweze
toa amri ya kuendelea kwa shauri hilo,ombi ambalo liliungwa mkono na Wakili wa Kujitegemea, Bw. Steven Kitale,
ambaye ni Mwenyeketi wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Kanda ya Mwanza.
Jaji Mashauri aliteuliwa
kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2019 nafasi aliyoshikilia hadi
kustaafu kwake. Kwa kipindi chote akiwa Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Mashauri ametoa
uamuzi mbalimbali katika mashauri ya jinai, madai na migogoro ya kazi na ardhi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni