·Akutana na kuteta na mwenyeji wake Prof. Juma
Na.
Faustine Kapama na Magreth Kinabo-Mahakama
Jaji
Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo leo tarehe 24 Mei 2022
ameanza ziara ya siku tatu kuitembelea Mahakama ya Tanzania kwa lengo la
kubadilishana uzoefu ambapo amekutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Wakiwa
ofisini hapo, viongozi hao wamefanya mazungumzo mafupi yenye lengo la kujenga
ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kimahakama na yale yanayohusu vyuo kuiwezesha
Mahakama ya Uganda kujifunza jinsi ya kuijengea uwezo Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama
nchini Uganda (JTI).
Mhe.
Owiny-Dollo, ambaye ameambatana na ujumbe wa maafisa 12 kutoka nchini Uganda alisema
kuwa wamekuja nchini Tanzania kupata maarifa na wanatumaini kujifunza mengi
kutoka katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na pia kupata uelewa
jinsi ya kuijengea uwezo wa Taasisi yao.
Kwa
upande wake, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa anashukuru kwa ugeni huo kwa kuja nchini kwa sababu wamekuwa wakikutana
Majaji Wakuu katika mikutano yao mbalimbali,
lakini hawajawahi kukutana kujadili kuhusu vyuo vyao vya uongozi na sheria
ili kubadilishana uzoefu.
“Hivi
karibuni tulikutana nchini Zimbabwe (majaji wakuu) kuzungumzia masuala ya
matumizi ya teknolojia na nadhani hili ni eneo jipya tunalotakiwa kwenda nalo,”
alisema Mhe. Prof. Juma ambaye aliambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi
wa Chuo na pia Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika.
Jaji
Mkuu wa Tanzania alibainisha kuwa tayari ameshakiagiza Chuo cha IJA kuandaa
kozi za kuwajengea uwezo maafisa wa
Mahakama ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
"Nimekiomba
chuo chetu kuangalia jinsi tunavyoweza kwenda kidigitali ili watusaidie katika
eneo hili. Mahakama haiwezi kubaki nyuma katika masuala ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwa Dunia na Serikali inatumia teknolojia hiyo,"
alisema.
Jaji
Mkuu aliueleza ujumbe kutoka Uganda kuwa Mahakama ya Tanzania imewashirikisha
wadau wengine katika mnyororo wa utoaji haki katika safari hiyo ya mabadiliko. Aliwataja
baadhi ya wadau hao kama Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa
Serikali(DPP), Jeshi la Magereza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Idara ya Uhamiaji,
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS) na
wananchi.
Naye
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo aliwakaribisha wageni hao Tanzania na
katika Chuo cha IJA ambapo aliwaahidi kuwa
wakiwa Lushoto watapata fursa ya kutembelea maeneo ya chuo na vivutio
mbalimbali vilivyopo katika Wilaya ya Lushoto.
Viongozi
wengine waandamizi walioambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania katika kuwakaribisha
wageni hao ni Mkuu wa Chuo cha IJA na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Paul
Kihwelo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina.
Miongoni
mwa viongozi walioambatana na Jaji Mkuu wa Uganda ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Uganda, Dkt.
Flavian Zeija, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi
wa JTI Uganda, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Msajili wa Taasisi
ya JTI Uganda na viongozi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria Uganda
(IDLO).
Katika
ziara yake, Jaji Mkuu wa Uganda anatarajia pia kutembelea maeneno mbalimbali ya
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na vivutio mbalimbali vilivyopo
katika Wilaya ya Lushoto.
Wakiwa
IJA, wageni hao watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na viongozi wa Chuo hicho
ikiwemo namna kinavyofanya kazi. Ziara hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya
Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uganda na ujirani mwema kati ya nchi hizi
mbili.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akisalimiana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Uganda, Dkt. Flavian Zeija.
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo (kushoto) alimkabidhi mwenyeji wake jarida (juu) na bendera ya Taifa la Uganda (chini) kama zawadi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni