Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba leo tarehe 23 Mei, 2022 amefungua mafunzo kuhusu
usikilizaji wa mashauri yatokanayo na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yanayowaleta
pamoja watumishi wa kada ya Kumbukumbu na TEHAMA kutoka katika Mahakama
mbalimbali chini Tanzania.
Katika hafla fupi ya ufunguzi huo, Mhe. Chaba
ameelezea imani ya Mahakama kuwa wote watakaopatiwa mafunzo hayo yanayoratibiwa
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Tanzania (IJA) kwa ufadhili wa Serikali ya
Uingeleza watakuwa chachu kwa wengine ili kuleta mabadiriko chanya kwenye
utendaji kazi.
“Mtakapomaliza mafunzo haya mkawe chachu kwa wengine
ili kuongeza imani ya wananchi juu ya uendeshwaji wa shughuli za Mahakama”
alisema. Mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika katika ukumbi uliopo ndani ya
jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki – Morogoro yanatarajiwa kumalizika tarehe
25 Mei, 2022.
Akisoma taarifa fupi kabla ya ufunguzi, Mkurugenzi
Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania. Bw. Stephen Magoha alisema kuwa
mafunzo hayo yanamanufaa makubwa kwani yatawasaidia watumishi kutumia muda mfupi katika usikilizaji wa
mashauri na kujifunza namna ya
urejeshaji mali zinazotokana na makosa ya rushwa.
Aliongeza, “Mbali na kuwaongezea uelewa wa
uendeshaji wa mashauri ya rushwa, ni matarajio yetu kuwa nyinyi mtaenda kuwa
walimu wazuri kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao hawajafanikiwa kupata fursa
ya kuhudhuria mafunzo haya.”
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba
akifungua mafunzo kuhusu usikilizaji wa mashauri yatokanayo na makosa ya rushwa
na uhujumu uchumi.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Messe Chaba (katikati), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Sylvester Kahinda (kushoto) na Mkurugenzi wa Mafunzo Stephen Magoha (kulia) wakifuatilia wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni