·Awaomba wananchi wasilalamikie kasi usikilizaji mashauri
Na.
Faustine Kapama-Mahakama
Waziri
wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro leo tarehe 23 Mei, 2022
amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake
jijini Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo mafupi ambapo ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji mkubwa wa utoaji huduma za haki kwa wananchi.
Akiongea
na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema
kuwa uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama, ikiwemo mifumo mbalimbali na
majengo umesaidia kuchochea utoaji wa haki kwa wananchi kwa wakati ambapo
ameshuhudia ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, utunzaji mzuri wa
kumbukumbu na nyaraka na pia utoaji wa huduma kwa njia za kidijitali.
“Kwa
yule anayeijua Mahakama jinsi ilivyokuwa kabla ya uboreshaji huu atagundua kuna
hatua kubwa imefanyika. Walioanzisha uboreshaji huu wanastahili pongezi. Labda
niwakumbushe kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa sasa, Balozi Hussein Katanga ndiye
aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa kwanza wa Mahakama na ndiye aliyeanzisha uboreshaji
huu. Amefanya kazi kubwa ambayo imeendelezwa na wale waliomfuatia. Kusema kweli,
Mahakama inastahili pongezi,” amesema.
Mhe.
Dkt. Ndumbaro amebainisha pia kwa sehemu ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama
unaenda sambamba na kuhakikisha mashauri yaliyopo mahakamani yanasikilizwa
ndani ya muda mfupi iwezekenavyo. “Kama ambavyo wanasema, haki iliyocheleweshwa
ni haki iliyodhurumika. Kwa hiyo, tusicheleweshe haki na Mahakama imeshafanya
hivyo na inaendelea kufanya,” amesema.
Kwa
mujibu wa Waziri huyo, kwa sasa shauri katika Mahakama ya Mwanzo linatakiwa
kuisha ndani ya miezi sita, katika Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi shauri
lazima liishe ndani ya miezi 12 na katika Mahakama Kuu isizidi miaka miwili,
hivyo amesema hata kama mashauri hayo yakiisha ndani ya siku moja hicho ndicho kinachotakiwa.
“Ile
habari ya kesi kukaa mahakamani miaka 10 imeisha sasa kwa sababu mtu ambaye anakwenda
mahakamani anadai haki, tunapomchelewesha tunachelewesha haki yake. Kwa hiyo,
niwaombe wananchi tusilalamike kwamba usikilizaji wa kesi unakwenda haraka
sana, tuiunge mkono Mahakama kwa hili ili anayedai haki aipate ndani ya muda
mfupi kadri inavyowezekana,” amesema.
Akizungumzia
kilichojiri kwenye mazungumzo yao, Mhe. Dkt. Ndumbaro amefurahi kupata fursa ya
kuitembelea rasmi Mahakama ya Tanzania akiwa Waziri wa Katiba na Sheria na kukutana
na Jaji Mkuu wa Tanzania, ambaye amemweleza jinsi gani Mahakama imefanya kwenye
uboreshaji katika utoaji haki, katika kuwafikia wananchi na katika kupata
mrejesho kutoka kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni